ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 22, 2010

Dhahabu yaua mkazi wa Tarime

MTU mmoja ameuawa kwa mapanga baada ya kuvamia na kupora mawe ya dhahabu katika Mgodi wa dhahabu wa North Mara uliopo katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Jeshi la Polisi kanda maalumu ya Polisi Tarime limethibitisha kutokea kwa mauaji hayo kwa vyombo vya habari jana. “ Inaonekana alipata dhahabu , wenzake wakamgeuka na kumuua kwa mapanga”, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Tarime , Constantine Masawe alisema jana asubuhi.

Alimtaja marehemu kuwa ni Mohere Biraro, mkazi wa Kijiji cha Kewanja kilichopo meta chache kutoka Mgodi wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya African Barrick Gold.

Tukio hilo lilitokea juzi mchana na kwamba marehemu aliokotwa barabarani akiwa amejeruhiwa vibaya kwa mapanga , kwa mujibu wa Kamanda Masawe. Juhudi za wasamaria kumkimbiza katika Hospitali ya Nyamongo kwa matibabu hazikufanikiwa, alisema Masawe.

Maofisa wa Polisi wameanza msako mkali dhidi ya waliohusika na mauaji hayo, alisema Masawe. “ Hadi sasa hukuna mtu aliyekamatwa lakini tunawasaka wahusika”, aliongeza Kamanda Masawe

No comments: