MAJAMBAZI wenye silaha zinazodhaniwa kuwa za kivita wamevamia Kituo Kikuu cha Wilaya ya Kipolisi ya Nyamwaga na kumimina risasi za moto katika ofisi zake na makazi ya maofisa wa polisi wanaoishi karibu na ofisi hizo.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Kipolisi Tarime, Constantine Masawe, amesema majambazi hao walivamia nyumba tatu tofauti zilizopo meta 20 kutoka kituo cha Polisi juzi saa tano usiku na kuwaweka watu chini ya ulinzi na kisha kuiba idadi kubwa ya ng’ombe na mbuzi wa eneo hilo.
Akiwafariji wananchi wa kijiji cha Nyamwaga jana asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Frank Uhalula ambaye aliitisha mkutano wa hadhara wa dharura, alisema ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba hakuna aliyejeruhiwa katika tukio hilo kwa sababu risasi hazina macho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa dharura, baadhi ya wananchi waliomba serikali kutafuta mbinu mbadala ya kukabiliana na wimbi la uhalifu katika Wilaya ya Tarime.
Baadhi ya wanakijiji hao walimwambia Uhahula kuwa polisi waliopo katika eneo hilo wana umri mdogo na hawana uwezo wa kubeba silaha nzito na kupambana na majambazi.
“Hao askari waliopo hapa ni watoto wadogo. Tunaomba askari waliokomaa na wenye uzoefu kupambana na majambazi,” alisema mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Francis Ghati.
No comments:
Post a Comment