Kenya imetwaa mataji yote kwenye mashindano ya ulimwengu ya mbio za Cross Country zilizofanyika Jumapili katika mji wa Bidgoszcz, nchini Poland.
Mkenya Joseph Ebuya ndiye bingwa mpya wa dunia wa mbio hizo za cross country za umbali wa kilomita 12, hii ikiwa ni mara ya kwanza Kenya kutwaa ubingwa wa mbio hizo katika kipindi cha miaka 11, tangu bingwa wa zamani wa dunia Paul Tergat aliposhinda mbio hizo mjini Belfast mwaka 1999.
Ebuya alikimbia kwa muda wa dakika 33 akifuatwa na Teklemariam Medhin wa Eritrea, naye Moses Ndiema Kipsiro wa Uganda akamaliza wa tatu.
Emily Chebet ndiye aliyeshinda mbio za wanawake za kilomita 8 akimpiku kwa sekunde moja Mkenya mwenzake, bingwa wa dunia wa mbio za mita 10,000 Linet Masai. Meselech Melkamu kutoka Ethiopia alishika nafasi ya tatu na kunyakua shaba.
Kwa upande wa vijana waKenya walichukua nafasi za kwanza nne upande wa wavulana na pia wasichana,na kuonyesha uwezo mkubwa wa kufanya vyema katika mashindano ya miaka ijayo.
No comments:
Post a Comment