ANGALIA LIVE NEWS
Wednesday, May 26, 2010
Aliyedondoka na ungo Dar
GUMZO limeibuka jijini Dar es Salaam na vitongoji vyake kuhusiana kuibuka kwa habari za mzee mmoja aliyedaiwa kudondoka na ungo katikati ya barabara saa kumi alfajiri maeneo ya Mbezi Mazulu wilayani Kinondoni.
Gazeti hili lina habari hiyo A to Z kutoka katika vyanzo vyetu mbalimbali ambapo ilidaiwa kuwa mzeee huyo alikutwa ameduawaa katikakati ya barabara inayotoka maeneo hayo kwenda Barabara ya Morogoro na mtu wa kwanza kumuona alikuwa dereva mmoja aliyekuwa akiendesha gari.
Habari zinasema dereva huyo alipofika sehemu hiyo alimuona mtu akiwa uchi na akiwa amekalia ungo uliosheheni vikorombwezo mbalimbali kama vile vibuyu, pembe, vitambaa, chupa na vingine ambavyo hakuweza kuvitambua. (angalia picha kubwa mbele).
Taarifa hizo zilidai kwamba baada ya dereva huyo kumuona mtu huyo alishituka ndipo alimpigia honi lakini aliendelea kukaa akigeuza geuza macho mithili ya kinyonga ndipo alipiga mayowe yaliyosababisha wapita njia na majirani wa eneo hilo kufika eneo la tukio .
Habari zaidi zilieleza kwamba kila aliyefika alishangaa kumuona mtu huyo ambaye alikuwa amejipaka rangi nyeusi sehemu mbalimbali za mwili wake huku akiwa na kipande kidogo cha nguo nyeupe kwenye makalio.
Habari zinasema wananchi walimhoji kutaka ataje jina lake, alikotokea na alikokuwa akienda ambapo alikataa kutaja jina bali aliwaambia kwamba alikuwa na wenzake wanne wakitokea Mkoa wa Shinyanga wakielekea Visiwa vya Shelisheli katika mkutano mkuu wa wachawi wa Bara la Afrika.
Aidha, ilielezwa kwamba mzee huyo alisema kwamba kwa Tanzania walifanya kikao chao mkoani Shinyanga ambapo waliteuliwa watano akaongea kuwa alikuwa anaamini alidondoka katika eneo hilo kutokana na maswala ya kiufundi.
Mtu huyo alisema baada ya ‘ndege’ yake kuanguka, wenzake waliendelea na safari wakiamini alikuwa akiitengeneza kisha angewafuata Shelisheli .
“Ndani ya ungo aliokuwa amekalia kulikwepo na pembe za mbuzi , kisu, vibuyu na chupa mbili zilizojazwa dawa na sanamu ya kuchonga mfano wa nyoka,” alisema shuhuda mmoja.
Habari zinasema kutokana na kuitikia wito wa polisi jamii, baadhi ya wananchi waliokuwa na namba ya simu ya Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kipolisi ya Kimara aliyejulikana kwa jina mmoja la Madaraka alipigiwa simu ili afike eneo la tukio.
Vyanzo vilidai kuwa pamoja na mkuu huyo wa upelelezi kupigiwa simu lakini ilichukuwa muda mrefu polisi kufika eneo la tukio hali iliyowafanya baadhi ya washiriki wa polisi jamii kumlaani kiongozi huyo kwani wananchi walianza kumpiga mzee huyo wakidai kuwa huenda ndiyo wachawi wanaowachukuwa watu Misukule.
Vyanzo hivyo vilidai kwamba mzee huyo alianza kupata kipigo huku baadhi ya wananchi wenye huruma wakiendelea kumpigia simu mkuu wa upelelezi wa Kimara ili aje kumuokoa bila mafanikio hadi alipokata roho ambapo vitu alivyokuwa navyo pamoja na ungo vilichomwa moto lakini inadaiwa havikuungua na asubuhi yake havikukutwa eneo la tukio.
Wananchi wengi waliohojiwa na gazeti hili katika eneo hilo walilalamikia jeshi la polisi hasa Wilaya ya Kimara na kusema kwamba wameonesha uzembe wa hali ya juu kwa tukio hilo, kwani wangeweza kuokoa maisha na kufanikiwa kupata mengi kutoka kwa mtu huyo kama wangemkuta hai.
“Marehemu hakuwa na kitu chochote cha kuweza kumtambulisha kwa jina au anakotokea wapi licha ya kusema kuwa anakwenda Shelisheli, … alikuwa na maandishi yaliyokuwa yakisomeka Tanzania,” alisema shuhuda huyo.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa polisi walikuja na kuchukua maiti ya mtu huyo ambayo hata hivyo haijulikani ilipopelekwa na hadi jana jeshi la polisi lilikuwa halijatangaza tukio hilo kubwa kwa jamii.
Baadhi ya wananchi walisikitishwa na kitendo cha kuuawa kwa ‘mtaalamu’ huyo kwani angeweza kuulizwa juu ya sayansi hiyo ya kusafiri kwa ‘ndege’ ya kichawi (ungo).
Waandishi wa gazeti hili walifika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kimara na kuulizia ilipo maiti ya mtu huyo lakini Kaimu Mkuu wa Kituo hicho aliyejulikana kwa jina la Madaraka aligoma kutoa ushirikiano na badala yake waliambulia kufokewa.
“Nyinyi kwani hamjui utaratibu wa jeshi la polisi, ondokeni hapa mtapoteza muda wenu bure,” alifoka Kamanda Madaraka.
Hata hivyo, waandishi waliwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Elias Kalinga ambaye alisema kuwa hajui ilipo maiti hiyo na kuahidi kuwa atafuatilia na angepiga simu katika chumba chetu cha habari lakini hadi tunakwenda mitamboni hakufanya hivyo.
Baadhi ya wananchi wamekuwa wakipiga simu katika chumba cha habari cha gazeti hili na kuhoji kwanini polisi hawajatoa taarifa juu ya mtu huyo anayedaiwa kuwa ni mchawi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment