MASHIRIKA yanayojishughulisha na masuhala ya Haki za binadamu, Usawa wa jinsia na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FEMACT) imesema imestushwa na kusikitishwa na matamshi ya Rais Kikwete juu ya kaulli yake aliyokaririwa na vyombo vya habari ya “Matukio ya mimba kwa wanafunzi wa kike nchini yanasababaishwa na viherehere vya wanafunzi wenyewe”.
Katika taarifa yao waliyoitoa jana jana katika vyombo vya habari na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Ananilea Nkya, Femact ilisema kuwa matamshi yake hayo yanapotosha juu ya swala la mimba mashuleni.
Femact ilidai kuwa hivi karibuni Rais kikwete alikaririwa kauli hiyo na taarifa hiyo kutolewa katika chombo cha habari cha kila siku Juni 7 mwaka huu na kumkariri kauli hiyo ya; “Matukio ya mimba kwa wanafunzi wa kike nchini yanasababaishwa na viherehere vya wanafunzi wenyewe”. Ambapo walidai inapotosha umma.
“Tunamsihi Rais atafakari ili matyamshi yake yasilete hisia za kupotosha umma kuhusu ukweli wa mambo ambayo Serikali inahitaji kuyafanyia kazi ili kutokomeza tatizo hilo linaloikabili nchi nzima hasa sekta ya Elimu.’ Ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia iliendelea kusema kuwa, ; Nidhahiri kuwa wananchi wengi hasa walioko pembezoni wana matarajio makubwa sana kwa Rais wao, ikiwa ni pamoja na kupigania haki na usawa kutokomeza aina zote za ukandamizaji,ubagauzi na na ukatili wa jinsia hasa kwa wanawake na watoto wa kike ambao ni waathirika wakubwa.
Aidha, FEMACT ilisema kuwa Rais kutoa kauli inayobwaga lawama kwa wanafunzi wa kike bila uchambuzi kunaenda kinyume na azma ya Serikali kuwajibika kwa wananchi kufanyia kazi matatizo ya msingi yanayosababisha wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari za serikali kupata ujauzito.
Ikifafanua zaidi juu ya Swala hilo, FEMACT ilisema kuwa , kwa mujubu wa Wizara ya Elimu, mpango wa Serikali kuhusu shule za Sekondari za Kata zijengwe karibu na makazi ya wananchi ili watoto kutoka nyumbani na kwenda shule na kurudi nyumbani kwa urahisi kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wengi wanapata elimu nzuri na bora zaidi….
hata hivyo walidai kuwa asilimia kubwa ya utekelezaji wa mpango huo haujafanyika ilivyokusudiwa kwa sababu kuna maeneo mengi nchini ambapo wanafunzi wengi tena wenye umri mdogo chini ya miaka 17, wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa kumi kila siku kwenda na kurudi shule huku wakipita katika mapori, mabonde na milima yenye hatari mbalimbali kwa maisha yao ikiwemo ubakaji.
Pia katika taarifa yao hiyo ,walidai kuwa sahule hizo za Kata hazina mpango wa kuwapatia wanafunzi usafiri , chakula, mabweni kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka mbali pia akuna walimu wa kutosha na mitaala ya ziada ikiwemo Michezo wala vitabu pamoja na maabara kwa ajili ya masomo ya Sayansi mambo ambayo yangevutia wanafunzi kupenda kujifunza na kuepuka vishawishi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment