ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 30, 2010

Mtanzania ahusishwa jaribio la mauaji ya jenerali Nyamwasa

OBURG, Afrika Kusini
south africaMTANZANIA mmoja ni miongoni mwa watu waliofikishwa mahakamani nchini Afrika Kusini kwa tuhuma za kuhusika katika jaribio la mauaji ya mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda, Luteni Jenerali Faustin Kayumba Nyamwasa mjini Johannesburg Juni 19.

Waendesha mashtaka nchini humo pia waliwafikisha mahakamani watu wengine raia wa Somalia na Msumbiji kwa tuhuma za jaribio hilo la mauaji, ambapo Nyamwasa alinusurika baada ya kupigwa risasi tumboni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari Afrika Kusini, ilielezwa mahakamani hapo kwamba watuhumiwa hao pia wana historia ya uhalifu na kukutwa na vifaa vilivyoibwa.

Baada ya kusomewa mashtaka dhidi yao, watuhumiwa hao kwa pamoja walirejeshwa mahabusu baada ya kesi yao kuahirishwa hadi mwezi ujao ili kuruhusu uchunguzi kuhusu uhalali wao kuwepo nchini humo utakapokamilika.

Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani baada ya polisi kuwaachia huru watuhumiwa wengine wawili wiki iliyopita, ambao pia walikamatwa kwa tuhuma za kuhusishwa na jaribio hilo la mauaji.

Luteni Jenerali Nyamwasa, kiongozi wa zamani wa jeshi la Rwanda aliyekimbilia uhamishoni mwezi Februari mwaka huu, alinusurika katika jaribio la kumuua Jumamosi Juni 19 alipokuwa akitoka kufanya manunuzi ya vifa vya nyuimabni akiwa na mkewe.

Nyamwasa alikimbilia nchini Afrika Kusini baada ya kutofautiana na mshirika wake wa muda mrefu, Rais Paul Kagame wa Rwanda baada ya kumtuhumu kwamba amekuwa akijihusisha na rushwa.

Mke wa Luteni Jenerali Nyamwasa, Rosette amekuwa akiilaumu serikali ya Rwanda akidai kwamba inahusika na jaribio hilo ambapo mtu mwenye silaha alimpiga risasi tumboni kisha kutoweka bila kuchukua kitu chochote.

Tuhuma hizo zimekanushwa na serikali ya Rwanda ambayo imekuwa ikimtuhumu Nyamwasa kwa kuhusika na milipuko ya mabomu iliyotokea mjini Kigali mwezi Februari na kuitaka serikali ya Afrika Kusini imrejeshe pamoja na Kanali Patrick Karegeya ambao kwa pamoja walikimbia nchini humo.

BBC

No comments: