ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 16, 2010

Tabia za wanaume wanaojipenda katika mapenzi!

Naamini utakuwa mzima wa afya njema na uwanja huu unaendelea kukujenga kila siku. Kama ndivyo ni furaha yangu. Mimi ni mzima, nipo kamili kukuletea mada itakayokuongezea mtazamo mpya katika faili lako la uhusiano.

Naam! Leo nataka kuzungumza juu ya mada ambayo itawagusa wengi sana. Wapo baadhi ya wanaume wanaojipenda sana kwenye jamii yetu. Utakuta mwanaume yupo ‘smart’ wakati wote, kila muda yupo mkanda nje!
Hawa ndiyo ninaotaka kuwazungumzia. Katika wanaume wa aina hii, wapo wa makundi mbalimbali. Hapa chini, kwanza nakuletea makundi hayo halafu tutaangalia tabia zao.

Kundi A
Hawa wanapenda kuwa wasafi muda wote, wakiwa makini sana na mavazi yao. Mara zote wanapenda kuvaa kiheshima na kuhakikisha kiatu hakikosi rangi! Hawa ni wale ninaopenda kuwaita mkanda nje!
Hapo namaanisha kwamba hupendelea kuvaa suruali za vitambaa na mashati ya kawaida. Mitindo yao ya nywele si ya kihuni, wananyoa saizi moja au staili nyingine zinazokubalika zaidi kwa watu wanaojiheshimu.

Kundi B
Hawa ni mabishoo, wasafi muda wote, wakitumia muda mwingi kutafuta manukato ya kunukia vyema na kuiga kila aina ya mitindo mipya inayoingia. Wanapenda kunakshi nywele zao.
Wakiingia saluni, hawaishii kunyoa tu, lazima wataweka wave, black na dawa nyingine kwa ajili ya kupendezesha nywele. Baadhi yao huenda mbali zaidi, hadi kufikia hatua ya kutoboa masikio.
Si ajabu kumkuta akiwa amefunga kitambaa kichwani. Unaweza kumuona kila siku ana gari jipya lakini kumbe hakuna hata moja ambalo ni mali yake. Yote ya kuazima! Miwani za rangi ni chaguo lao jingine, cheni kubwa shingoni nayo ni pambo lao kuu. 

TABIA ZAO
Suala la usafi, kujipenda na mitindo ni kitu cha kawaida na kizuri pia kufanywa na mtu. Ukiwa mtanashati unapendeza, unavutia na unaficha umaskini. Huu ndiyo ukweli ambao wengi wanakubaliana nao.

Wanaume wa kundi la kwanza, asilimia kubwa ni wastaarabu na wanaojipenda tu. Huwa ni wacheshi na wanaokubalika na wengi, lakini bila kujijua wamekuwa wakiwatesa wanawake wengi zaidi kimapenzi kwa vile wanavutia na wanaonekana wastaarabu!
Kama mwanaume huyo hatakuwa makini, ni rahisi sana kujikuta ameshawishika na kuingia katika uhusiano na wanawake tofauti tofauti kwa kipindi kifupi. Hata hivyo, wanaume hao wanatajwa kama watu makini, wenye misimamo.

Pamoja na hayo, wanajikuta wakishindwa kusimamia misimamo yao wakati mwingine, kutokana na kusifiwa sana na wanawake, hivyo kujikuta wameshaanguka katika penzi ambalo hawakulitarajia!
Ndani ya muda mfupi tu, anajikuta ameingiza msururu wa wanawake kwenye ‘list’ yake ya aliotoka nao kimapenzi. Mara nyingine huingia wenyewe kwenye mitego bila kujijua, maana utafiti usio rasmi, unaonesha kwamba wanaume hawa ni wacheshi sana, hasa kwa kuwatania (kuwachokoza) wanawake, zaidi wanapokuwa katika sehemu zao za kazi. 

Hivyo basi, utani ukizidi wanajikuta wameshaingia mapenzini, lakini baada ya kufikiri kwa muda wanagundua kwamba, hawakupenda bali walitamani tu!
Kundi la pili ni aina ya wanaume ambao wengi wao hufanya hivyo kwa lengo la kupata wanawake kirahisi zaidi. Wanaume hao huwa tayari hata kutoka na wanawake wanaowazidi umri, kikubwa wanachozingatia ni fedha! Utanashati wao unawavutia wengi, hivyo kwao kutoka na mwanamke mpya kila siku si ‘story’ kivile, maana wengi wanajigonga wenyewe.

WANA MAPENZI YA DHATI?
Mapenzi ya kweli yapo kwenye moyo wa mtu, kwahiyo wanaume hawa pia wana mapenzi na wapo ambao kwao ni kila kitu. Wanaweza kupenda na kuwa na uhusiano imara kabisa, ambao unaweza kuzaa ndoa hapo baadaye.

Yapo mambo mawili ya kuzingatia; Kwa wanaume wa aina hii, wawe makini sana na wanawake, kwani mvuto wao ndiyo unaowachanganya na kujikuta wengi wakiwaweka kwenye mitego.
Wanawake ambao wapo kwenye uhusiano na wanaume wa aina hii ni vizuri wakafahamu kwamba, wapo kwenye mapenzi na wanaume ambao wanapendwa na wasichana wengi, kwahiyo wawe wabunifu zaidi kwenye mapenzi, lakini si hivyo tu, bali wahakikishe wanachunga mizigo yao! Kama vipi hadi wiki ijayo.

Wasiliana na Joseph Shaluwa kwa ushauri au maoni kupitia HYPERLINK “mailto:joeshaluwa@yahoo.com” joeshaluwa@yahoo.com au mtembelee kwenye blog yake www.shaluwanew.blogspot.com kwa makala zaidi na mambo ya mapenzi.

No comments: