ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 21, 2010

Namna ya kuanzisha uhusiano mpya!

HELLO ladies and gentlemen! I hope kila kitu kinakwenda sawa, maisha yanasonga na mipango inapangika. Mimi nipo mzima kabisa, tayari kuja na somo kama linavyoonekana hapo juu. Imekaa poa, au siyo wakubwa zangu? Haya pamoja sana! 
Kwa majuma mawili mfululizo, nimekuwa nikieleza somo la kupoteza uwezo wa kuwa na mwenzi mmoja, halafu na njia za kuanza mazoezi ya kuelekea kwenye upya na kurudi kwenye hali ya kawaida ya kupenda mwenzi mmoja tu.

Ni somo lililowasaidia wengi. Niliwasiliana na wengi, ambao walisema wazi wazi jinsi walivyopata tiba hiyo nzuri kwa maisha yao. Walifurahi sana, maana walikuwa kama watumwa. Mtu mmoja, wapenzi saba, sio kwa kupenda, ni ugonjwa!

Kama nilivyosema, kupoteza uwezo wa kuwa na mwezi mmoja ni tatizo ambalo dawa yake niliitoa katika mada hiyo. Hapa sasa, nataka kukufundisha mbinu za kisasa, bora zitakazokufanya uanzishe uhusiano mpya wenye nguvu na utakaozaa ndoa hapo baadaye.

Wengi hupaparika sana katika hatua hii, wanashindwa mahali pa kuanzia. Kila kitu kinakuwa kigumu kwao, wanakosa uwezo wa kujua ni nani hasa anafaa na nini cha kufanya katika uhusiano huo mpya.

Kumbuka mada hii ni mwendelezo wa wale waliokuwa na tatizo la kupoteza uwezo wa kuwa na mwenzi mmoja, weka hiyo kichwani ili usichanganyikiwe katika vipengele vinavyofuata.

Sasa, unajua cha kufanya wakati wa kusaka mwenzi wa kuingia katika uhusiano mpya? Vipengele vinavyofuata ni dawa tosha kwako. Hebu twende tukaone;
JIKAGUE...
Kitu cha kwanza kabisa rafiki zangu, kabla ya kuingia kwenye mchakato wa kuwa na mwenzi lazima ujikague kwanza. Jiridhishe kama ni kweli umebadilika. Huna tena matatizo uliyokuwa nayo awali.

Kama unadhani bado hujawa sawa, jipe muda zaidi wa kuwa ‘single’ kwanza ili siku ukianzisha uhusiano unakuwa wenye nguvu zaidi.
Jiulize, ni kweli sasa upo tayari kuingia kwenye penzi jipya? Penzi la mwezi mmoja tu? Ni kweli? Moyo wako umesharidhia kabisa kuwa katika uhusiano na mwenzi mwaminifu. Je, ni kweli kwamba sasa unaweza kuhimili hisia zako na kutumia muda wako vizuri na si ngono? Kama ukijiridhisha vyema katika maeneo hayo, kipengele kinachofuata hapa chini kinakuhusu sana.

JIONYE!
Usisubiri kuambiwa, wakati mwingine ili ubadilike, lazima wewe mwenyewe uchukue hatua ya kujionya. Jiambie mwenyewe: “Sasa natakiwa kubadilika, sitaki tena wapenzi wengi, kwanza ni kujishushia heshima. Nataka kuwa salama katika penzi la mwenzi mmoja.”

“Sitaki kuitwa majina mabaya, sitaki kuwa malaya tena. Nataka kuwa mpya sasa. Nitajitunza na kuufanya mwili wangu kuwa wa mtu mmoja tu, ambaye nitaingia naye katika ndao.”
Ni maneno mazito sana, yenye uwezo wa kupanda kitu kipya ndani ya moyo wako.
CHUNGUZA WENZI WALIOPITA
Baada ya hatua iliyopita, kabla ya kuanza kuwaza mtu mpya, ni vyema pia ukageuka na kutazama wale uliokuwa nao awali. Nilishauri uachane nao wote ili uweze kupata tiba vizuri.

Utafiti unaonesha kwamba, wanaokuwa na wenzi zaidi ya mmoja, wapenzi wao huwa hawajui kama wapo na mtu ambaye ana uhusiano mwingine! yaani hata kama una wapenzi tisa, kila mmoja anaendelea kuamini kwamba yupo peke yake!
Kwa maneno mengine wanakuwa na mapenzi ya dhati huku wakiwa na malengo mbalimbali. Sina shaka kati yao, kuna ambaye anakukuna zaidi. Hilo linawezekana.
Lakini pia, siyo ajabu kabisa kuwa kati yao hakuna ambaye unaweza kumpa nafasi tena.
Wachunguze, kama yupo anayekidhi, mpe nafasi, kama hakuna twende katika hatua nyingine hapa chini...
ANZISHA URAFIKI UPYA
Usiwe na papara, hapa unashauriwa kuanzisha urafiki sana na watu wa jinsi tofauti na yako. Usielewe viabaya tafadhali, nisema uanzishe urafiki wa kawaida na jinsi tofauti na siyo mapenzi.

Kwanza utajifunza tabia zao, watakuwa wawazi kwako, utajua vitu wanavyopenda. Watakupa siri zao nyingi. Watakuasimulia jinsi walivyo na mwisho wa siku utafanya uchaguzi mzuri, maana angalau sasa utakuwa unajua unakwenda kuingia katika uhusiano na mtu wa aina gani.

CHAGUA KWA MAKINI
Usifanye makosa, fanya uchaguzi wako kwa makini sana. Kati ya rafiki zako, angalia ambaye anakidhi hasa kuwa na wewe. Hapa unatakiwa kuhakikisha kwamba, hata mambo yake hayatakuboa maana ni mtu ambaye unamfahamu vizuri sasa.
Ukimuona tu, anza kuwa naye karibu zaidi ya wengine ukizidi kumchunguza na vitu vingine vya ndani zaidi. Uliza kuhusu magonjwa ya kurithi, tabia za kabila lao, mila n.k

Hapa atakuambia ukweli, maana atakuwa anakuchukulia kama rafiki tu, hatakuwa na sababu ya kukuficha kitu. Atakuwa mkweli kwako mpaka hatua ya mwisho. Usipojua mila zao ni hatari, maana inawezekana kwao, ukiolewa/kuoa si vibaya kutembea na shemeji yako!

Ni vizuri kuchunguza haya mapema, ili ukianza uhusiano unakuwa upo kamili. Nafasi yangu haitoshi, hapa naweka kituo kikubwa halafu wiki ijayo tutaendelea na vipengele vingine pamoja na kuwapa dawa za kumshawishi rafiki yako huyo, akubali kuwa kwako.

Next issue!!!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake; www.shaluwanew.blogspot.com 

1 comment:

Anonymous said...

DJ LUKE UNAMAMBO HAYA