ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 26, 2010

Waziri apiga magoti, atoa shikamoo akiomba kura


Waziri wa Maliasili na Utalii, Tanzania Shamsa Mwangunga

Waandishi Wetu, Dar na mikoani

MBIO za kuwania ubunge na udiwani kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimezidi kuonyesha vioja, burudani na ufundi wa kampeni, baada ya jana Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga, kutoka na mbinu yake mpya ya kuwapigia magoti wapigakura.

Waziri Mwangunga ambaye amekuwa akikabiliwa na  upinzani mkali kutoka kwa mwanasiasa kijana na machachari Nape Nnauye, ambaye ni mtoto wa  mwanasiasa mkongwe marehemu Brigedia Moses Nnauye, alitoa mpya hiyo ambayo pia ilifanywa na mgombea mwingine Hawa Ngh'umbi. 

“Mimi nimewahi kuwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji na nimekuwa mbunge wa viti maalumu kwa Mkoa wa Dar es Salaam kwa vipindi viwili na sasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kura zenu shikamooni CCM,” anaripoti Musa Mkama, kutoka Dares Salaam.

Tukio hilo la aina yake lilitokea kwenye kata ya Makuburi jijini Dar es Salaam saa 9:30 asubuhi, ambapo waziri huyo alitenda hayo bila kujali umri, huku upande mwingine ikielezwa kuwa ndiyo staili yake ya kuonyesha unyenyekevu  kwa Chama na wanachama wa Chama hicho, kwamba ndivyo atakavyowatumikia akiwa mbunge wa jimbo hilo.

Wakati hayo yakiendelea, mgombea mwenzake yaani Ng’humbi, aliulizwa swali na mwananchi ambalo hata hivyo mwenyekiti wa kikao hicho cha kujinadi wagombea kwa 13 wa jimbo hilo, alimzuia kulijibu kwa kile alichokieleza kwamba lilikuwa nje ya mada.

Baada ya mgombea huyo kuzuiwa kujibu swali la mwananchi huyo, palitokea kutoelewana kwa dakika kadhaa huku mwananchi huyo akishinikiza kujibiwa kwa swali lake, kwa sababu  alizodai ni haki yake ya kikatiba na ndiyo sababu yupo hapo.

Swali la mwananchi huyo lilikuwa:, "wewe wakati upo UWT kulitokea wizi wa fedha na wewe ulikuwa ni mmoja wao, baadhi yao wakapelekwa mahakamani, hivyo unawezaje kuturudishia imani sisi kwamba, wewe unaweza kuongoza jimbo hili kwa umakini na usitokee wizi kama ule?"

Lakini, hali hiyo ya kutoelewana , ilitulia na wagombea wakaendelea kujinadi ingawa wengine waliomba kuorodhesha mlolongo wa wafisu wao (CV)  huku dakika chache walizopewa zikiisha bila  kuomba kura.


CHANZO:MWANANCHI

No comments: