
Kabla sijaendelea nitoe shukrani zangu kwa wote ambao wamekuwa wakiwasiliana nami na kutoa pongezi zao kutokana na kazi ninayoifanya. Kiukweli kabisa mnanipa sana moyo wa kuendelea kufanya vizuri zaidi na zaidi.
Naam, mada ninayoizungumzia ni sifa kumi nyeti ambazo ni kivutio kikubwa kwa wanaume kutoka kwa wanawake. Inawezekana umeshakutana na mada hii sehemu nyingine, lakini hapa nitakufafanulia kwa mapana zaidi ili uweze kupata mwanga na kufurahia maisha yako ya kimapenzi.
Wiki iliyopita nilianza na kipengele cha kwanza kabisa ambacho ni kuwa na penzi la dhati. Sasa endelea kupitia vipengele vingine hapa chini.
PILI: Kuheshimu thamani yake. Kuna tofauti ya mwanamke na mke, kila mwanamke ni mwanamke kwa sababu ana jinsi ya kike, lakini mwanamke huyo huyo, inawezekana kabisa akashindwa kuwa mke, kama akikosa sifa za kuwa mke.
Kati ya sifa muhimu sana ambazo mwanamke anayetaka kuwa mke anatakiwa kuwa nazo ni pamoja na kuheshimu thamani yake. Mwanamke anayeheshimu thamani yake, kama mwanamke halisi mwenye maadili, anajiweka katika nafasi nzuri ya kuwa mke!
Ninaposema kuheshimu thamani, ninakuwa na maana kubwa sana, thamani yako ni unyenyekevu, kuwa msaidizi wake wa karibu na kujishusha kwa mpenzi wako. Ikiwa utaanza kuonesha sifa hizi katika uchumba, unakuwa unampa sababu za kufikia kukuchukua moja kwa moja kama mke.
Wengi huwaza, ikiwa katika uchumba tu, unakuwa mkali, mkorofi, usiye na mapenzi na sifa zote mbaya, je ukiingia kwenye ndoa itakuwaje? Jitahidi sana uwe na sifa hii.
TATU: Heshima. Wanaume wanapenda kuheshimiwa. Ukiweza kumheshimu mpenzi wako, unakuwa umejikatia tiketi tena ya siti ya mbele kabisa ya kuelekea kwenye ndoa. Heshima ninayoizungumzia hapa si ile ya kumpigia magoti au kuonesha woga muda wote utakaokuwa naye, la hasha! Namaanisha heshima ya kutambua kwamba huyo ni mumeo mtarajiwa, ambaye kama maandiko matakatifu yanavyoweka wazi kuwa ndiye kichwa cha nyumba!
Utakuta mwingine hachagui maneno ya kuzungumza na mpenzi wake, litakalokuja kichwani analitoa kama lilivyo, hana haja ya kuchuja. Hili ni tatizo. Chunguza kila neno moja unalotaka kulitoa kwa mpenzi wako, kama kweli unamheshimu huwezi kutoa kauli chafu.
Acha tabia ya kurushiana maneno machafu na mpenzi wako, kuwa na staha na upime kila unalotaka kumwambia mpenzi wako. Hakuna mwanaume anayetaka kuishi na mwanamke ambaye watakuwa wanashindana ndani, hakuna anayetaka mke ambaye ana mdomo mchafu.
Hana heshima, anamchukulia mpenzi wake sawa na shoga yake wa mtaa wa pili; hili ni tatizo. Lazima uchukue hatua na ufanye mabadiliko ya dhati kabisa, kama ni kweli unahitaji kuingia kwenye ndoa.
NNE: Anayejitambua. Kujitambua kunaposemwa katika kipengele hiki, ni kule kujifahamu kuwa wewe ni mwanamke na unatakiwa kufanya nini kwa mumeo mtarajiwa. Kama nilivyotangulia kusema katika vipengele vilivyopita, ni lazima umpe sababu mpenzi wako ya kuwa na wewe, kujitambua ni kati ya sababu hizo.
Usifanye mambo kwa kusukumwa au kuagizwa. Mara nyingi vitu vya kufanya kwa kuagizwa huwa vinafanyika huku mtu akihisi kama ameonewa au anapelekeshwa. Jitume, fanya mambo yako mwenyewe bila kulazimishwa.
Mathalani umeshinda kwa mpenzi wako, amerudi kazini jioni, unamuona hana furaha, hana tabasamu, unatakiwa kufahamu kwamba yupo katika matatizo. Lakini hupaswi kumuuliza kwa kumkaripia. Zungumza naye kwa sauti ya upole, umwulize tatizo ni nini?
Ujue kwanini amepoteza furaha yake, wewe uwe kama mlezi wake, unayetaka kujua tatizo alilokabiliana nalo siku hiyo. Hapo utakuwa umemsaidia sana na kwa hakika utakuwa umejiongezea sifa za kuwa mke wake mtarajiwa.
TANO: Aliye mfariji! Maisha yana changamoto mbalimbali, nzuri na mbaya, nyepesi na nzito! Sasa unapokutana na changamoto ngumu, wakati mwingine unaweza kupoteza furaha yako, hata ufanisi wako wa kazi unaweza kupungua.
Katika hali hii, lazima anayekabiliwa na changamoto hizo apate mfariji, mtu wa karibu yake ambaye atamwambia hayupo peke yake katika mapito hayo. Mpenzi/mke/mume ndiyo wanaoaminika zaidi kuwa na nguvu ya kuweza kurudisha furaha ya mwenzake iliyopotea.
Itumie nafasi hii kumfariji, kwani kufanya hivyo kunazidisha sababu kwa mwenzi wako, kuona kabisa kwamba ana sababu za kukufanya mkewe maana kama ni faraja ataipata nyumbani na si kwa marafiki.
Naweka kituo kikubwa hapa, hadi wiki ijayo tena kwa mwendelezo wa mada hii nzuri itakayobadilisha fikra zako.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake; www.shaluwanew.blogspot.com
No comments:
Post a Comment