
NAAM kama ilivyo ada tumekutana tena kwenye kona yetu ya mahaba, ili kujuzana machache kuhusiana na maisha yetu ya kila siku ambayo yametawaliwa na mapenzi kwa asilimia kubwa.
Nina imani waumini wote wa dini ya kiislamu wapo katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Wote walio katika mfungo wa mwezi huu nawatakiwa mfungo mwema.
Mmoja wa wasomaji wa kona hii aliniuliza swali juu ya uamuzi wake wa hasira kwa mpenziwe uliopelekea watengane na baadae kugundua alifanya pupa kutoa maamuzi ya kuachana na mpenzi. Na alipoomba msamaha alikataliwa, swali likaja afanyeje na yeye mpenzi wake bado anampenda.
Swali mmelisikia kilichobakia ni majibu ambayo kila mtu anajibu lake ambalo naamini litakuwa tofauti na mwenzake. Lakini kwa upande wangu swali hili nitalijibu kwa kina ili tujue tatizo lipo wapi si kutibu matawi tukasahau mizizi.
Kumekuwapo na matatizo mengi katika uhusiano kwa watu kukwazana kufikia hatua ya kutoleana maneno makali yatakayo pelekea mmoja kuvunja mahusiano. Siku zote mtu unapokuwa na hasira maamuzi mengi huwa njia ya mkato. Mwenye hasira hutoa uamuzi wa kitu chochote kwa jazba bila kuangalia madhara yake.
Mwenye hasira yupo tayari kufanya chochote bila kuangalia madhara yake ni nini, siku zote muamuzi ukiwa na hasira sehemu kubwa ni kuharibu kuliko kutengeneza. Hata vitabu vya Mungu vimesema shetani hukuvaa wakati ukiwa na hasira na baada ya tendo huondoka na kujikuta umefanya jambo la ajabu.
Hebu angalia watu wote waliotenda mambo yao kwa hasira hakuna hata mmoja aliyefanya kwa faida zaidi ya hasara na kujutia walichokitenda baada ya tukio. Presha inapokuwa juu huwezi kutoa uamuzi wenye busara kwani busara inahitaji muda na hasira aihitaji muda zaidi ya maamuzi ya mkato.
Napenda kulizungumzia hili pale unapopandwa na hasira jiepushe sana kutoa uamuzi, hata kama umeudhika vipi, Siku zote lazima ujue kuzidhibiti hasira zako. Swali utazidhibiti vipi?
Linapotokea tatizo ambalo litakuudhi usipende sana kubishana kwa muda mrefu kitu ambacho kitakupandisha munkali na kufikia hatua ya kupigana au kutoleana maneno machafu.
Unaweza kuidhibiti hali hii kwa kunyamaza au kuondoka eneo la tukio, kwani wapo ambao huwakwaza wenzao kwa makusudi ili afanye alilolikusudia.
Linapotokea tatizo kaa chini na kutafakari tukio zima unaweza kukuta tatizo lililopo halikuwa na ukubwa wa mfarakano wenu na kuamua kuachana nalo. Hata kama mkeo/ mumeo/ mpenzio mmekoroshishana ni jambo la kawaida katika dunia, jaribu kutumia busara kujiepusha na shari ambayo ukiipa nafasi mwisho wake huwa wa majuto na kusema ningejua wakati umeishachelewa.
Napenda kumalizia kwa wote ambao wapenzi wao walitoa maamuzi mazito baada ya kukwaruzana na kufikia hatua ya kutengana, lazima tuelewe sisi wanadamu tuna udhaifu wetu na makosa ni sehemu ya kujifunza.
Kama mpenzio amegundua kosa lake na kukuomba msamaha ni nafasi yako ya kumsamehe huku ukimueleza makosa yake ambayo hatakiwi kuyarudia na kama atarudia hapo lazima ujue yote aliyoyafanya alifanya kwa kudhamiria na una uamuzi wowote.
Lakini tusisahau bado mpenzi wako ana nafasi kusamehe saba mara sabini lakini yakizidi akili kichwani. Siku zote asiye na mapenzi ya kweli humuadhibu mpenzi wake kwa kutumia kosa alilofanya.
Ukiona mpenzi wako unamuomba msamaha na ameng’ang’ania msimamo wake ujue ulikuwanaye kama kivuli tu lakini hakuwa mwenzako katika safari ya huba. Usiumize kichwa fungua ukurasa mwingine.
No comments:
Post a Comment