
Mpenzi msomaji wangu, kama wewe ni mfuatiliaji wa karibu wa safu hii utakumbuka wiki iliyopita nilizungumzia umuhimu wa wapenzi kuheshimu imani za wenzao hasa katika kipindi hiki.
Nilimaanisha kwamba, mmoja wenu anapokuwa Muislamu na akawa anafunga, mpenzi wake lazima awe na moyo wa subira, isiwe sababu ya yeye kumsaliti kwa kuwa na mtu mwingine.
Hata hivyo, baada ya kuandika makala hayo, nilipokea ‘sms’ na simu nyingi kutoka kwa wasomaji wakiniuliza maswali kuhusiana na makala hayo na nilifanikiwa kuwajibu moja kwa moja kadiri nilivyoweza.
Ninachotaka kusisitiza kuhusiana na mada hiyo kabla ya kuingia katika kitu kingine ni kwamba, hisia za wapenzi wetu zisiwe sababu za kwenda kinyume na imani za dini zetu.
Mpenzi wako anapokulazimisha kufanya na wewe mapenzi kwa maelezo kwamba amezidiwa na hawezi kukusaliti kwa kwenda kwa mtu mwingine, huku akijua wazi ni dhambi kubwa hasa katika kipindi hiki, huyo huna sababu ya kuendelea kuwa naye.
Nijuavyo mimi kama mtu ametokea kukupenda kwa dhati, lazima ataiheshimu imani yako na atakuwa tayari kusubiri badala ya kukushawishi ‘umpatilizie’.
Niseme tu kwamba, mapenzi yapo kila siku, mwezi mmoja siyo kipindi kirefu hivyo tusikubali kwenda kichume na imani zetu kwa sababu ya wapenzi wetu.
Endapo mpenzi wako atakuwa akikushawishi kufanya yale ambayo ni kinyume, huyo atakuwa ni shetani, mpotezee!
Baada ya kugusia kidogo mada ya wiki iliyopita, sasa nirudi katika kile nilichodhamiria kukiandika wiki hii. Msomaji wangu kutoka Tanga aliyejitambulisha kwa jina la Raheem aliomba ushauri juu ya suala moja ambalo katika kumsaidia nimeona bora niandike mada itakayowasaidia wengi.
“Mimi na mpenzi wangu wote ni Waislamu, nampenda sana na natarajia siku moja tutakuja kuishi kama mke na mume Mungu akipenda. “Kinachonikera ni tabia ya mpenzi wangu huyu kutokutaka kufunga. Yaani yeye anavyoishi hana tofauti na siku za nyuma, nguo anazovaa ni za kimitego, nikijaribu kumshauri abadilike anasema kama naona hanifai, nimuache.
Sitaki kumuacha lakini pia sifurahishwi na mwenendo wake, naomba unishauri,”anasema Raheem.
Katika maisha ya kimapenzi hakuna kitu kinachowaumiza walio wengi kama kuingia katika uhusiano na baada ya siku chache, penzi kunyauka kama siyo kufa kabisa.
Wapo walioolewa juzi juzi tu lakini maskini ya Mungu leo hii ninapoandika makala haya wameshaachwa. Achilia mbali hao ambao wamechukua muda mfupi kabla ya kuachana, wapo ambao wamekuwa pamoja kwa muda mrefu na kufanyiana mengi mazuri lakini leo hii imebaki stori, tena kwa hawa inauma zaidi kwakuwa yawezekana mizizi ya penzi lao ilishakwenda mbali, huku kila mmoja akiwa ameshajijengea katika akili yake kuwa amepata mtu wa maisha yake kumbe hamna kitu.
Leo nataka niseme kitu kimoja, naamini kwa wale watakaosoma watajifunza. Asilimia kubwa ya wazazi wetu wako hai na wengi wao hadi leo wako pamoja na wanaishi maisha ya furaha na amani licha ya tofauti za hapa na pale ambazo zimekuwa zikijitokeza. Kuna siri kubwa ya wapenzi na wanandoa kudumu katika uhusiano wao kwa muda mrefu.
Uvumilivu! Hakika kama wewe huna moyo wa uvumilivu ni vigumu sana kudumu na huyo uliyenaye na usipokuwa makini kesho au kesho kutwa unaweza kufanya maamuzi ya kumwacha mpenzi wako wakati bado unampenda.
Mpenzi wako anaweza kuwa na udhaifu flani, yawezekana akawa anafanya mambo ambayo wewe hayakufurahishi lakini wakati huo huo unampenda, kikubwa ni kumvumilia na kwenda naye taratibu huku ukijaribu kumrekebisha kwa kutumia lugha ya upole.
Hakikisha udhaifu wa mpenzi wako hauwi sababu ya nyie kukorofishana mara kwa mara bali kubaliana na hali hiyo kwanza kisha ndipo uangalie njia sahihi za kumbadilisha. Naamini kwamba, kama kweli anakupenda atakusikiliza na kubadilika ili kutokukwaza. Lakini asipobadilika, uamuzi utakuwa ni wako, kusuka au kunyoa.
Ni kweli uvumilivu una mwisho na kuna mambo mengine ambayo ni vigumu kuyavumilia lakini linapokuja suala la mapenzi, jaribu kuwa na moyo wa ujasiri kidogo wa kutokuwa tayari kumkosa kirahisi mtu uliyetokea kumpenda eti kwakuwa tu anafanya mambo yasiyokufurahisha.
Elewa kwamba yawezekana hata wewe kuna mambo ambayo mpenzi wako hayapendi lakini anakuvumilia akijua ipo siku utabadilika, ndiyo maana nasema kuna kila sababu ya kuvumiliana ili uhusiano wetu uweze kudumu.
Kwa leo nilitaka kufikisha ujumbe huo.
Tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine
No comments:
Post a Comment