ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 29, 2010

Lipumba aongoza kuharibikiwa magari

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza na wananchi waliohudhuria moja ya mikutano yake.
Na Mwandishi Wetu
Katika Wagombea Urais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania, watatu ndiyo wanapewa nafasi kubwa kutokana na mtaji wa kisiasa walionao lakini mmoja wao anatia fora kwa kuzimikiwa na magari.

Tathmini ya Risasi Mchanganyiko, ina majibu kuwa tangu kuanza kwa kampeni za kisiasa kwa wanaowania Urais, Ubunge na Udiwani Agosti 20, 2010, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Lipumba ndiye anakabilikiwa na matukio ya kuharibikiwa na magari katika mikutano yake kuliko wengine.

Lipumba ambaye ni mmoja kati ya Wagombea Urais watatu wenye nguvu, amewahi kuharibikiwa na magari mara mbili na matukio hayo kuripotiwa na vyombo vya habari, wakati alipokwenda kwenye ziara za kuomba kura kwa wananchi mikoa ya kusini.

Wakati kwa Lipumba ikiwa hivyo, kwa wagombea wengine wawili waliosalia wenye nguvu, Rais Jakaya Kikwete (CCM) na Dk. Wilbroad Slaa (CHADEMA), wamekuwa wakiendesha kampeni zao kwa raha mustarehe pasipo bughudha.

Hata hivyo, uchunguzi wa Risasi umebaini kuwa kikubwa ambacho kinawafanya Slaa na Kikwete kutokumbwa na matukio hayo ni aina ya usafiri wanaoutumia ambao una tofauti kubwa na ule wa Lipumba.

Slaa na Kikwete wamekuwa wapasua anga kwa kutumia helkopta, isipokuwa katika maeneo machache, wakati Lipumba yeye usafiri wake muda mwingi ni wa gari, hivyo kukumbwa na masahibu hayo.
Ubovu wa barabara ni pointi nyingine ambayo imemfanya Lipumba akumbwe na misukosuko ya kukwama njiani, hivyo kuchelewa kuwafikia wapigakura wake.

Pamoja na hali hiyo, Risasi lilizungumza na baadhi ya wananchi ambao walimshauri Lipumba kufikiria upya kutumia usafiri wa helkopta ili kuendana na kasi ya wenzake.

“CUF ni chama kikubwa kuliko CHADEMA, kinapokea ruzuku nyingi kuliko CHADEM, hii inashangaza kinashindwa kuwa na ubunifu wa kufanya kampeni kwa helkopta wakati CHADEMA kimeweza. Kingine hata magari, kinatakiwa kuangalia yale magari yenye ubora,” alishauri mkazi wa Mwenye, Jamal Hamdun.

Mwananchi mwingine, mkazi wa Sinza, Anna Douglas alisema: “Isifikiriwe kwamba kutumia helkopta ni ufisadi, badala yake ionekane hiyo ni njia ya kusaidia kuwafikia wananchi kwa urahisi. 

Lipumba ana rekodi ya kugombea Urais tangu mwaka 1995, kwahiyo uzoefu wake ungemsaidia kujua kwamba usafiri wa anga hasa helkopta ni muhimu kwa kipindi hiki kwa sababu gari peke yake litasababisha maeneo mengi asifike.”
Chanzo:Global Publishers

No comments: