
Baada ya mfungo, kila mmoja ana haki ya kufurahia kile alichokifanya kwa kutegemea radhi za Allah.
Leo wapendwa nimekuja na mada inayohusu ahadi zisizotimia hasa kutokana na tukio lililojitokeza siku ya sikukuu kama hii mwaka jana.
Rafiki yangu alishindwa kumtimizia ahadi ya kumnunulia nguo za sikukuu mpenziwe, lakini kama ilivyo siku zote mwanadamu hupanga yake na Mungu hupanga yake.
Mambo yalimuendea vibaya rafiki yangu mpaka siku ya sikukuu inafika hajatimiza ahadi, kitu kilicholeta mgogoro ndani ya nyumba. Hata siku ya sikukuu jamaa alikuja na wageni, kilichomkuta ni aibu mkewe hakugusa jiko ilibidi jamaa awapeleke wageni hotelini, kwani mwanamke hakupika kisa mumewe hakumtimizia ahadi aliyoahidi.
Na unyumba umekuwa tabu, akimgusa usiku anaambulia matusi imefikia hatua mkewe analala na nguo kisa zawadi.
Swali linakuja ni ahadi hiyo hiyo au kuna kitu kingine? Je, unampenda mpenzi wako yeye alivyo au mpaka awe na kitu fulani au zawadi ndizo zinazolinda penzi lenu?
Japo ahadi ni deni lakini lazima ujue kuna kupata na kukosa, na mapenzi ya kweli hayalindwi na kitu bali nyinyi wenyewe. Zawadi ni matokeo na inapokosekana haipunguzi chochote katika mapenzi yenu.
Inapofikia hatua ya kumnyima haki yake ya ndoa eti sababu hajatekeleza alichoahidi, hapo unakuwa umevuka mipaka ya mapenzi. Inajionyesha unampa haki yake kwa gharama na si upendo wa dhati toka moyoni mwako.
Siku zote inapotokea hitilafu ndani ya ndoa, iwe siri yenu hata wageni wakija wasijue mpo kwenye hali gani. Mwanamke mwelevu huficha siri ya ndani ili mgeni asijue.
Ni kweli umekasirika kukosa kitu ulichokisubiri kwa hamu, lakini ndivyo hivyo hakikupatikana. Japo umeudhika lakini hilo usiliingize kwenye mapenzi. Unapoombwa haki ya ndoa, itoe tena kwa nguvu zote kuonyesha unampenda mpenzio si kwa kitu bali yeye mwenyewe na umalizapo kumtoa kijasho chembamba una nafasi ya kumueleza.
“Mpenzi umeniudhi,” naye ataeleza sababu zilizopelekea kutotimiza ahadi yake. Ili kuonyeza mapenzi ni kumjali mpenzio katika hali yoyote hata mkiudhiana, usiku unapoingia ukiguswa usiweke kisasi cha kumjibu maneno ya kifedhuli “Ooh, unikome” au “Achana na mimi”
Unapoitwa na mpenzio itikia wito, mwenzio ameshikika mpe haki yake ili kuongeza mapenzi na kujionyesha unampenda yeye mwenyewe alivyo wala siyo kitu.
Unatakiwa kuwa farijiko la mwenzako, anapokosa usimlaumu bali mpe moyo kwa kuamini kama kakosa leo basi atapata kesho.
Mwisho namalizia kwa kusema, penzi la kweli halilindwi na uzuri wa mtu wala fedha bali upendo wa dhati ambao hauna gharama yoyote zaidi ya kujitoa kwako.
Kwa haya machache tukutane wiki ijayo.
Na Ally Mbetu
Simu: +225 713 646500
E-mail: ambedkt@yahoo.com
No comments:
Post a Comment