19th September 2010
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbeya kimejibu mapigo ya wapinzani wake baada ya kuwatahadharisha wananchi wa Jimbo la Mbeya Mjini kutofanya majaribio kwa kumchagua mwanaume aliyetoga masikio na mvaa hereni awe mwakilishi wao bungeni.
Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi Mbeya Mjini, Athanas Kapunga, ametoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge jimbo la Mbeya Mjini, Benson Mpesya, uliofanyika katika mtaa wa Kagera kata ya Ilomba.
Kapunga ambaye alikuwa Meya wa Jiji la Mbeya katika Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji hilo, alisema itakuwa ni ajabu kwa wananchi wa Mbeya watakapomchagua mtu aliyetoga masikini akawe ndiyo mwakilishi wao bungeni.
Katibu huyo wa Siasa, Itikadi na Uenezi ingawa hakumtaja moja kwa moja lakini maneno hayo yalikuwa yakimlenga mgombea ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Mr. 11 ambaye ameonyesha upinzani mkali dhidi ya mgombea wa CCM, Mpesya.
Alisema mgombea huyo wa Chadema anatoa ahadi kwa wananchi kwamba atagawa kompyuta bure kwa shule zote za sekondari wakati shule hizo anazoahidi kutoa msaada huo zimejengwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi.
Aliongeza kuwa wagombea wa Chadema wameeneza uvumi kuwa mke wa mgombea ubunge kupitia CCM, Benson Mpesya, amepooza miguu wakati siyo kweli na kuwataka wananchi kupuuza maneno hayo ambapo muda mfupi alikwenda kuchukuliwa mke wa Mpesya na kuonyeshwa hadharani.
Kwa upande wake mgombea ubunge jimbo la Mbeya Mjini kupitia CCM, Benson Mpesya, akizungumza katika mkutano huo aliwaponda wagombea wenzake wanaodai kuwa hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano katika jimbo hilo .
Mpesya alisema mgombea ubunge wa Chadema, Mbilinyi alikuwa mwanafunzi wake katika shule ya sekondari Mbeya Day lakini alitimuliwa akiwa kidato cha pili hivyo kama wananchi wa Mbeya ni wajanja wangefuatilia kujua ni kwanini alifukuzwa shuleni hapo.
No comments:
Post a Comment