ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 28, 2010

DONDOO SABINI zinazoimarisha mapenzi

BILA shaka wapenzi wasomaji wa safu hii mu wazima wa afya na kwa wale Wakristo natumaini mlisherehekea vyema Sikukuu ya Noeli.

Kama hivyo ndivyo, hatuna budi kumshukuru aliye juu kwa kutufanya tuendelee kuvuta pumzi ya bure. Kama ilivyo ada, hapa huwa tunazungumzia mapenzi na uhusiano. Katika mada hii tutazungumzia  dondoo 70 zinazoimarisha mapenzi.


KUKUMBATIANA: Hili ni tendo muhimu  kwa wapenzi kufanyiana kwa vile huongeza hali ya kila mmoja kuhisi kuthaminiwa na wakati huo huo hutafsiri ukaribu na uwajibikaji wa kila mtu kwa mwenzake.

UJUMBE WA MAPENZI: Inaweza isiwe sms ya simu hasa, lakini inaweza kuwa ni kuandika sehemu maneno yatakayolenga kufikisha ujumbe kwa umpendaye kuwa unampenda. Kitaalamu ujumbe huwa na nguvu kubwa zaidi hata ya maneno.

MAWASILIANO: Moja kati ya mambo muhimu kwenye mapenzi ni mawasiliano, hakikisha kuwa unakuwa mwepesi wa kuwasiliana na mwenzako asubuhi,  mchana wakati wa kazi na usiku. Mhamasishe umpendaye aamke, afanye kazi kwa bidii, ale chakula na mwisho umpumzishe kwa kumwambia “Lala salama mpenzi wangu”

UTANI: Kuna watu ambao huendesha maisha ya mapenzi kwa umakini au ‘seriasinesi’ kama wasemavyo wenzetu kiasi kwamba huwezi kusikia hata wakitaniana na wapenzi wao, hili ni jambo baya. Utani  ni mzuri kwa wapenzi kwani huondoa hofu na kusogeza ukaribu zaidi, lakini pia ni huburudisha.

MATEMBEZI:  Ni jambo zuri kwa wapenzi kuambatana pamoja katika matembezi yao. Kitendo hiki hujenga hali ya kila mmoja kujiamini kama siyo kujivunia chaguo lake mbele za watu.

KUKUBALI KOSA: Kwenye mapenzi  kuna wakati wa kukosana katika hili na lile, sifa ya wapenzi wa kweli ni kuwa tayari kuomba radhi kila inapotokea hali ya kutoelewana. “Nisamehe mpenzi wangu” Neno hili lisiwe la upande mmoja tu bali ni kwa kila mtu bila kujali huyu ni mwanaume au mwanamke.

KUTAMKA NAKUPENDA: Kila wanapokutana wapenzi kila mmoja awe tayari kufungua pazia lake la upendo na kutamka kwa kinywa “NAKUPENDA.” Hiki ni kiapo cha uaminifu kwa tafsiri nyingine, ndiyo maana hata wakati wa ndoa lazima maneno fulani yatamkwe na wanandoa.

DEKEZA: Tabia ya kupeana nafasi ya kudekezana ni nzuri katika mapenzi, wakati mwingine mwache mwenzako adeke mbele yako na wewe uwe tayari kwa moyo safi: “Mpenzi mi nataka unilishe” Ee..kauli kama hizi zinafaa kujenga mapenzi kwa wapendanao, haifai kuwa ‘magume gume’ wakati wote.

KUSIKILIZA: Unapokuwa na mpenzi wako sehemu na yeye akawa na neno la kukuambia hebu msikilize kwa makini na uoneshe kweli anachosema unakielewa, isiwe anaongea huku wewe umetazama pembeni au unachezea simu.

UAMINIFU: Nguzo kuu ya mapenzi ni uamifu, ni suala la lazima wapendanao
kuwa waumini wazuri wa uaminifu. Isiwe nakupenda mdomoni lakini kwa mwingine kuna udanganyifu na usaliti mwingi.

LAWAMA: Kuna watu wanapenda sana kuwalaumu wapenzi wao hata kwa mambo madogo madogo: “Kwa nini umechelewa kunifungulia mlango?” Anauliza hivi huku akiwa kanuna. Lawama hazifai kwenye mapenzi.

Inapotokea hali fulani isiyoeleweka kaa chini na mwenzako umuulize kabla ya kumlaumu pengine kuna sababu za msingi.

MACHO: Macho yanatabia ya kutafsiri yenyewe vitu vilivyopo ndani au kwa lugha ya kisaikolojia hufafanua zaidi maisha ya ulimwengu wa ndani. Macho ya wapendanao ni lazima yabebe ujumbe wa ndani, haiwezi kuwa ni kutazamana usoni kama bundi na nyoka. Unapotazamana na mwenzako legeza macho yako kuoneshe penzi lililoko ndani yako.

PONGEZI: Kama mwenzako amefanya jambo zuri mpongeze kwa kumwambia jinsi alivyokufurahisha, usifurahi moyoni mwako na kudhani kumsifia ni kumpa kiburi hiyo si kweli. Kakufanyia/kaifanyia jamii jambo jema mpe pongezi zake.

OFA YA MSAADA: Mwenzako anapokuwa na shida ambayo kwa upande mwingine unaifahamu usisubiri akuambie uitatue, kama una uwezo wa kufanya hivyo mpe ofa hiyo kwa kumshtukiza: “Uliniambia huna kodi ya nyumba mwezi huu, naomba twende nikakulipie.” Amini usiamini ukifanya hivyo utakuwa umemfurahisha mwenzako kwa kiwango kikubwa.

UTOAJI TAARIFA: Inapotokea sababu za kuchelewa, kutorudi nyumbani au kutotimiza ahadi fulani ni vema kutoa taarifa kwa mwenza wako, kufanya hivi kunaongeza uaminifu na kuondoa viashiria vya kupuuza na usaliti ambavyo ni vibaya kuachwa vichipuke.

Mada hii inaendelea wiki ijayo.

No comments: