MMILIKI wa kiwanja kilicho jirani na hoteli maarufu ya Palm Beach iliyoko jijini Dar es Salaam ambaye Serikali imemtaka abomoe ukuta wake kwa kuwa ni eneo la wazi, ametishia kumshtaki Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, akidai kuwa analimiki eneo kihalali.
Mmiliki huyo alikutana jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa anakusudia kumshtaki Waziri Tibaijuka kwa kuwa ameidharau Mahakama.
Mmiliki huyo, Taher Muccadam alisema Waziri Tibaijuka amedharau amri ya mahakama kwani alishinda kesi mahakamani na kuruhusiwa kuendelea na ujenzi katika kiwanja hicho.
Alisema kiwanja hicho namba 1,006 kilichopo Upanga anakimiliki kihalali na kwamba ana uthibitisho na vielelezo vyote vinavyomhalalisha kumiliki eneo hilo.
“Tibaijuka awe makini sana, hasa anapotaka kufanya maamuzi. Anaweza akaisababishia hasara Serikali kwa kulipa fidia,”alisema Muccadam.
Alisema eneo hilo si kiwanja cha wazi bali ilipendekezwa tu lakini, baadaye Manispaa ya Ilala ilitoa hati namba 186164/25 kwa wamiliki wa kwanza ambao ni Shantaben Narottambahi Patel na Nilaben Girishumar Patel mwaka 1975.
Alisema Desemba 6, 1975, Wizara ya Ardhi iliwazuia wamiliki hao kukiendeleza kiwanja hicho kwa sababu kilitakiwa kiwe cha wazi na kwamba waliahidiwa kiwanja mbadala namba 1019 kama fidia.
Muccadam aliendelea kueleza kuwa lakini, kiwanja hicho namba 1019 walichotakiwa kupewa wamiliki hao, kilichukuliwa na kumilikishwa kwa AMREF.
"Baadaye wizara iliamua kuwaruhusu waendeleze kiwanja chao cha zamani kwa kuacha upana wa futi 20 kati ya barabara ya Magore na Upanga.
Katika mkutano huo Muccadam alionyesha vielelezo mbalimbali kuhusu kiwanja hicho, ikiwemo barua ya Kaimu Kamishna wa Ardhi F. Luvanda yenye kumbukumbu namba LD/75708/101/LK ya Mei 25 mwaka 2005.
Katika barua hiyo, Kamishna huyo alipendekeza kuwa ili kumaliza mgogoro huo, kiwanja hicho kigawanywe na wamiliki wapate sehemu ya kuendeleza kwa matumizi ya ofisi na hoteli na eneo lingine libaki wazi.
Kwa mujibu wa Muccadam, tayari amemwandikia barua Waziri Tibaijuka kumjulisha suala hilo lakini hakuijibu barua hiyo wala hataki kukutana naye.
Alisema alinunua kiwanja hicho ili ajenge jengo la ghorofa 22, lakini tangu wakati huo, ameshindwa kuanza ujenzi kutokana na kuwepo kesi mbalimbali mahakamani kubishania kiwanja hicho.
Muccadam alisema mwaka 2000, kiwanja hicho kilifutwa kwa makosa, hivyo suala hilo lilipelekwa Mahakama Kuu na kufunguliwa kesi namba 70/2004 na baadaye Wizara ya Ardhi ilipendekeza mgogoro umalizwe nje ya mahakama.
Alisema aliendelea na malumbano hayo Mahakama Kuu kwa muda wote huo na hatimaye alishinda kesi na kurudishiwa kiwanja hicho na kwamba mahakama ilikubali alipwe fidia ya dola za Marekani 6 milioni kama gharama za ujenzi huo.
Katika hatua nyingine mmiliki wa kiwanja namba 1072 kilichoko Upanga Magharibi jijini Dar es Salaam kinachodaiwa kuwa hakina sifa ya kuwa kiwanja, amedai kuwa waziri Tibaijuka amedanganywa na watendaji wake kuhusu umiliki wa kiwanja hicho.
Paul Anthony aliliambia gazeti hili jana kuwa alipewa ‘ofa’ ya kiwanja hicho na wizara ya Ardhi tangu Januari 24, 1989 na kwamba ameendelea kukilipia kodi hadi leo.
Alisema kiwanja hicho kiko katikati ya viwanja viwili vilivyopimwa vya Salender Bridge Club na uwanja wa shule ya Muntazir lakini, kiwanja chake hakijapimwa hadi leo.
“Mkurugenzi wa Makazi ana ajenda ya siri juu ya kiwanja changu na jana (juzi) alimdanganya Waziri,”alieleza Anthony.
Alisema kabla ya kutakiwa kupewa hati, wizara ilimtaka kwanza atoe maelezo ya tathmini ya athari za mazingira kuhusu Mikoko iliyoko nje ya kiwanja hicho na alifanya hivyo.
Mmiliki huyo alionyesha vielelezo mbalimbali zikiwemo barua zilizoandikwa na J. Kombe kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) na ile ya Mali Asili na Utalii iliyoandikwa na Dk Tango kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Barua hizo zimeeleza kuwa kiwanja hicho kiko nje ya msitu wa mikoko na kwamba mradi unaotaka kutekelezwa hautakuwa na madhara yasiyoweza kudhibitika.
Barua hizo zilielekeza upimaji wa kiwanja hicho usisitishwe kwa kigezo cha kuharibu mikoko kwani kiwanja chenyewe hakina mikoko.
Alisema pia mchoro wa mipango miji namba 1/504/569 Dar es Salaam Area 2 ambako ndiko kiliko kiwanja chake bado haujaidhinishwa hali inayochangia kuchelewa kupimwa kwa kiwanja hicho.
Juzi Waziri Tibaijuka alitoa siku 30 kwa wananchi waliojenga nyumba kwenye maeneo ya fukwe ya Bahari ya Hindi kuzibomoa kabla ya kuanza kuchukua hatua.
Akizungumza katika ziara ya kukagua hali ya makazi na mipango miji katika jijini la Dar es Salaam jana, Waziri Tibaijuka alisema viwanja vya Serikali vilivyokuwa wazi haviruhusiwi kuwa makazi watu kwa kuwa viwanja hivyo ni kwa ajili ya michezo na bustani za kupumzika wananchi wa maeneo husika.
“Nasikitika kusikia kuwa wananchi wanaoishi hapa wamenunua maeneo haya. Hivi viwanja si vya watu ni vya Serikali na kila aliyenunua anapaswa kubomoa na kurudisha kiwanja kwa wahusika,” alisema Profesa Tibaijuka.
Alisema miongoni mwa viwanja hivyo ni eneo la wazi lililopo Ocean Road ambalo lilikuwa linamilikiwa na Shree Hindu Mandal, kiwanja namba 59 kitalu 1 kilichokuwa kinatumika kuchomea maiti mwaka 1952 mpaka 1967 na kuhamishiwa Kijitonyama na kutaka eneo hilo lilirudi mikononi mwa serikali.
Alisema katika hali ya udanganyifu Shree Hindu Mandal waliibuka na kudai mabadiliko ya matumizi ya kiwanja hicho na baadaye kupewa kibali na rais cha kutaka matumizi ya awali yafutwe na msajili alikifuta kwa nyaraka namba 131942 ya Septemba 2 mwaka huu kisha kuagiza manispaa ya Ilala ivunje ukuta uliopo.
Katika eneo jingine lililopo Palm Beach kiwanja namba 1006 ambalo lilikuwa la matumizi ya wazi mwaka 1975 kabla ya kubatilishwa kuwa eneo la mtu binafsi mwaka 2002 na mpaka sasa kinamilikiwa na mtu huyo.
“Mtu hawezi akajenga kwenye eneo la serikali kubwa kama hili wakati wananchi wanaoishi katika maeneo haya hawana sehemu ya kupumzikia wala sehemu ya watoto kucheza. Hii ni hujuma na wahusika wanapaswa kuchukuliwa hatua,” alisema Tibaijuka.
Alisema kiwanja namba 1072 kilichopo eneo la Upanga ambacho ni cha nyongeza, kilibuniwa pasipo kufuata utaratibu. Alisema kiwanja hicho kiko eneo la mikoko na hakijawai kupimwa rasmi.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment