ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 10, 2010

Usijihukumu, bado una thamani kubwa - 2

TUMEKUTANE tena kwenye kona yetu ya mahaba ili kujuzana machache kuhusu maisha yetu ya kila siku. 

Nashukuru kuona kona hii inasomwa na watu wengi na kupata maswali mengi kila kukicha ikiwemo ushauri wa kuiboresha. Hii imekuwa ikinipa moyo hata mimi muandaaji kuona kweli nikiandikacho kinaeleweka.


Leo tunaendelea na kiporo chetu tulichokiacha wiki iliyopita, nina uhakika bado cha moto na kinafaa kuliwa. Baada ya kuelezea jinsi ya kujitambua na kujiamini, leo tutazungumzia upande wa pili wa shilingi.

Baada ya kujitambua na kujiamini lakini umefika na kukuta siyo yule uliyemdhania au hajakupokea kama mlivyokuwa mkizungumza kwenye simu na kutokuwa tayari kuwa na wewe, ufanye nini?

Hapa kidogo pagumu kwa mtendewa kama alikuwa tayari alijitoa kasoro na kukutana na asichokitarajia cha kuonekana hafai. Hapa lazima atanyong’onyea na kukosa raha na kujiona hana thamani duniani.

Nini cha kufanya?

Lazima ukubaliane na matokeo kwa kujua kwamba kuna matokeo mawili kupata au kukosa. Hata hao unaowaona wazuri mbele ya macho yako na kuwaona hawawezi kukataliwa na wanawake, kuna sehemu hugonga ukuta.

Hata wanawake wazuri nao wana sura wanazozipenda hasa sura za kiume ambazo wewe unaona sura mbaya. Huwa hawapendi kuolewa na wanaume wazuri kwa kuhofia kushindwa kujitofautisha nao pindi wavaapo suruali.

Usishangae kupata mwanamke ambaye kwako utaona ni ndoto lakini ukweli unabakia palepale kila kilicho chini ya jua kina thamani kwa watu wake.

Makosa makubwa tunayofanya siku zote ambayo mwisho wa siku yanatugharimu ni kumuumba mtu akilini na kuamini unavyomfikilia ndivyo alivyo. Pia kuandaa ukaribu bila kujuana kwa sura umbile wala tabia.

Wapo watu kazi yao ni kutafuta wapenzi kwa njia ya mawasiliano na akisha mpata basi huachana naye kwa vile huo ndiyo utamaduni wake. Watu wa aina hii hawaangalii hali ikoje zaidi ya kukidha haja zake za mwili.

Tukija kwenye pointi yetu, umekutana na dhahama ya kukataliwa na mpenzi wako mliyepanga mengi kabla ya kuonana, ufanye nini?

Unachotakiwa ni kukubaliana na kilichotokea ili ujipange upya kwa kuamini uliyemchagua hakuwa sahihi kwako, hivyo basi badili utaratibu wa kutafuta mpenzi si kwa mawasiliano tena bali kwa kuonana na kupanga mipango kila mmoja amjue mwenzake. Namalizia kwa kusema kujiamini ndiyo njia pekee ya kukufanya uonekane mtu mbele ya watu.

Kwa leo hapa panatosha tukutane wiki ijayo kwa majibu ya swali lingine, kama una swali usisite kuuliza kupitia anwani zinazoonekana katika ukurasa huu.

No comments: