
WAKAZI wa Kitongoji cha Kazaroho, Kijiji cha Matui, wilayani Kiteto, mkoani Manyara wanaishi maisha ya hofu na kushindwa kufanya shughuli za maendeleo kwa kuogopa nyoka aina ya chatu anayetishia maisha yao kwa zaidi ya miezi mitatu sasa.
Kufuatia hofu hiyo, wameomba serikali kupitia idara ya wanyamapori, kumsaka nyoka huyo na kumuondoa kwenye makazi yao.
Wakazi hao walidai kuwa, nyoka huyo anayekadiriwa kuwa na uzito wa kilo 80, amekuwa akifanyiwa tambiko na wenyeji wa Kabila la Warangi na Wagogo kwa kumpa unga na maziwa, ili asilete madhara ndani ya kijiji hicho.
Mmoja wa wakazi hao, alisema nyoka huyo ana zaidi ya miezi mitatu kijijini hapo na wazee maarufu walipomuona, walitaka wananchi wasimdhuru kwani kuna masuala ya mila walitakiwa kufanya.
"Kwa kipindi chote hicho, makabila ya Warangi na Wagogo wamekuwa wakishughulika naye, lakini baada ya kuanza shughuli za kilimo watu wamepata hofu kubwa huenda akaleta madhara kwa jamii," alisema.
Akithibitisha kuwepo kwa nyoka huyo, Diwani wa kata hiyo, Kidawa Othmani (Obama), alisema tayari amewasiliana na maofisa wa maliasili ili wamuondoe.
Othman alisema kutokana na malalamiko ya wananchi kuwa, hawawezi kuamini usalama wao wamemtaka kutoa taarifa ili nyoka huyo aondolewe kijijini hapo sio kuuawa.
"Kwa kweli hali sio shwari hasa kipindi hiki cha kilimo, kila mtua anataka kwenda kufanya kazi zake maporini, sasa wanapokutana na nyoka huyo mara kwa mara inawatisha,” alisema.
Alisema hadi jana, maofisa hao walikuwa hawajafika na ametaka serikali inapojulishwa kuhusu hatari ndani ya jamii kufanya haraka kabla ya madhara.
"Nimeongea nao mwenyewe asubuhi (maofisa wa maliasili), wakaniahidi wanakuja lakini hadi hii jioni (jana) hawajafika, hali hii inaweza kubadilisha matokeo,” alisema.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment