ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 11, 2011

Dondoo Sabini Zinazoimarisha Mapenzi - 3

Safari yetu ya kutazama dondoo sabini za kuboresha mapenzi yetu ingali ikiendelea kwa mafanikio,  kwani kuna watu wengi ambao wamekiri kujifunza mambo ya msingi kwenye somo hili.

Labda ombi langu ni kwamba, kila tunalojifunza ni vizuri tukalifanyia kazi ili tuwe wapya katika mapenzi kila siku. Twende pamoja tena leo tutazame baadhi ya vipengele vya kunogesha mapenzi yetu.


LIKIZO: Mkiwa wapenzi mnaofanya kazi ni mnashauriwa kuwa na likizo ya pamoja itakayowafanya msafiri kutoka eneo mnaloishi na kwenda sehemu nyingine kwa lengo la kupumzika au kuwaona ndugu.

Kwa watu ambao si wafanyakazi suala la mapumziko halikwepeki, kwani ni muhimu kuwa na mapumziko ya pamoja ambayo yatawafanya muache shughuli zenu na kupumzisha miili na akili.

KISS: Kuna wapenzi ambao humaliza wiki, mwezi au hata mwaka bila kukiss na wenza wao. Kiss ni nzuri kwa sababu huvuta hisia pia ni utambulisho wa mapenzi yako juu ya mtu au kitu unachokibusu. Zingatia aina zote za kiss na umfanyie umpendaye.

TABASAMU: Mpendwa msomaji wangu, tabasamu ni ishara ya furaha ya ndani, hivyo unapokuwa na mwenza wako usiwe na uso wa ‘mikunjo’ kila wakati, bali onesha tabasamu lako hasa pale unapopata muda wa kutazamana na mwenzako.

MAVAZI: Ukiwa na mpenzi jaribu kukoleza hisia zake za mapenzi kwa kumnunulia nguo spesho ambazo zitamfanya aonekane mwenye mvuto mbele za watu. Kila ufanyavyo hivyo na yeye akazivaa na kusifiwa na wengine kuwa amependeza, jambo hilo litamfanya mwenzako akukukumbuke na kuongeza upendo kwako. Unadhifu ni suala zuri kwenye mapenzi.

ELIMU: Inapotokea mmoja wenu akawa na amesoma mahali jambo lenye faida katika mapenzi yenu amshirikishe mwenzake na ikiwezekana wasome kwa pamoja. “Ona mpenzi kuna makala hii nzuri ya mapenzi imeandikwa na Anko Rich hebu isome.”

HUISHA MAZUNGUMZO: Unapokuwa kwenye mazungumzo na mpenzi wako pendelea kurudia alichosema mwenzako kwa lengo la kuyazingatia aliyokuambia, kabla ya kujibu: “Ok nikamuone mama kesho? Nitakwenda mume wangu isiwe na shaka.” Mazungumzo ya namna hii humfanya mwenzako ajivununie usikivu wako.

SALAMU: Huwa nashangaa kusikia baadhi ya wapenzi hasa wale wanaoishi pamoja wakisema hakuna haja ya kusalimiana asubuhi eti kwa sababu wamelala pamoja, hilo si jambo jema ni vema kila siku asubuhi kusalimiana. Hii ni ishara pekee ya kumjali mwenzako.

UINGILIAJI: Kuna wakati ambapo mtu huwa na kazi au mipango yake binafsi ambayo anaifanya. Katika hali ya kawaida ni muhimu wazo lake au kazi ziheshimiwe. Inapotokea ulazima wa kumuingia ni vema kumuomba ruhusa kuliko kuvamia na kutoa amri.

“Naona unashona kofia, unaweza kuniazima dakika moja nikutume ukaniletee chaji yangu ya simu ndani?” Ukipendelea kufanya hivyo mpenzi wako atakuwa anajisikia furaha. Epuka kumkatiza kazi zake kwa: Unafanya nini hapo hebu nenda…”

KADI: Kutumiana kadi za pongezi na zenye jumbe mbali mbali ni utamaduni wa kimagharibi ambao tmerithi, lakini kwa kipindi hiki una nguvu sana katika kuimarisha mapenzi. Kuwa mtu wa kumtumia kadi mpenzi wako, kumtakia birthday njema n.k.

CHAKULA: Upishi na manunuzi ya chakula  anachikipenda mwenza wako ni dondoo nyengine nzuri ya kuongeza mapenzi. Usiwe mtu wa kupika au kununua chakula asichokifurahia mwandani wako.

ANAVYOJISIKIA: Unapokuwa kwenye mapenzi na mtu jaribu kuwa na utamaduni wa kumuuliza mwenzio jinsi anavyojisikia kuwa na wewe na kama kweli maisha ya mapenzi yanakidhi hitaji la moyo wake.

“Ni mwaka sasa umepita tangu tumekuwa wapenzi, hebu niambie unajisikiaje kuwa na mimi, nakutosheleza au kuna sehemu nakukasirisha?”
 Pokea ushauri wake na uufanyie kazi.

No comments: