
MTAZAMO: Unapokuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mtu, pendelea zaidi kuuliza mtazamo wa mwenzako kuhusu mwenendo wa maisha yetu. Hata unapotaka kufanya jambo fulani muulize mwenzako: “Nimefikiria twende likizo hii bila watoto, wewe unaonaje?
MUZIKI: Ni wazi kwamba muziki unatoa ujumbe na mafundisho. Inapendeza kwa wapenzi kuwekeana nyimbo zenye ujumbe wa mapenzi thabiti. Unapokuwa na mwenzako chumbani muwekee muziki laini na umwambie: “Sikia wimbo huo mpenzi wangu…tambua kwamba ni ujumbe wangu kwako.”
MANDHARI YA DUNIA: Ukitafakari juu juu unaweza usione faida ya kutafakari pamoja mandhari zuri ya dunia, lakini mkiwa pamoja kwenye fukwe ya bahari mkitazama machweo ya jua bila shaka mtafurahia utukufu wa Mungu pamoja. Tembeleeni bustani na mbuga za wanyama pamoja.
MICHEZO: Ni jambo jema kwa wapenzi kucheza pamoja michezo mbalimbali, mfano karata, kuruka kamba na hata kunyang’anyana vitu, kutupiana mito na mambo kama hayo. Lengo ni kufurahi pamoja kama wapenzi.
MAFUNDISHO: Mpe nafasi mpenzi wako akufundishe mambo anayofahamu. “Sijui kabisa kuhusu programu hii ya kompyuta, unaweza kunifundisha mpenzi wangu?” Kufundishana hujenga msingi wa kutegemeana na kuaminiana kuhusu uelewa wa mambo.
ULIZA VICHOCHEO. “Mpenzi najua uko mbali na mimi lakini hebu jaribu kufikiria ningekuwa karibu yako ungependa nikufanyie nini kati ya mambo yafuatayo; kukukumbatia, kukubusu mdomoni, kukushika kiunoni?” Mchombeze mwenzako kwa maneno ya namna hiyo siyo anapokuwa mbali bali hata hata kama uko naye.
Mazungumzo ya namna hiyo husisimua mwili.
MAVAZI YA KUFANANA: Ninaposema mavazi ya kufanana simaanishi suti, lakini hata nguo za kawaida, kwa mfano mwenza wako anaweza kuwa na traksuti nyeupe na fulana nyekundu na wewe ukavaa traksuti ya njano na fulana nyekundu, kisha mkatembea barabarani. Hakika mtapendeza na kuwa kivutio kwa watu.
MAJONZI: Tumekwisha eleza umuhimu wa kusaidiana katika maisha, lakini mwenzako anapokuwa na tatizo linalomsumbua si vibaya kama utamuuliza kuhusu msaada wako. “Pole mpenzi, lakini nimepanga kukusaidia sijui wewe unasemaje?” Wakati mwingine ni vizuri kusikia mpenzi wako akiomba msaada, kuliko kujitokeza na kumsaidia kwani inawezekana hakutegemei.
NDOTO: Vipi kuhusu ndoto. Umewahi kumuuliza mwenzako ameota nini usiku? Siku moja jaribu na ikiwezekana mshirikishe kile ulichoota. Kitaalamu ndoto ni wingi wa kumbukumbu zilizotunzwa akilini.
Hebu fikiria kuhusu usemi huu: “Nimeota tuko pamoja yaani nilikuwa nasikia raha sana.” Bila shaka, licha ya kuwa ni ndoto lakini utafurahi kusikia ulimfurahisha kupitia njozi.
Itaendelea wiki ijayo, usikose kumalizia dondoo hizi kwenye gazeti hili la Uwazi.
No comments:
Post a Comment