“NDIYO, ni miaka mitatu imepita tangu nivamiwe nyumbani kwetu usiku wa manane nikiwa nimelala ndani mimi na wenzangu watatu, nikakatwa mguu wangu wa kulia na kunyofolewa kabisa na vidole vitatu vya mkono wangu wa kushoto, bado sijasahau tukio hilo, ndiyo maana nasema siwezi kwenda nyumbani kwetu, sipapendi, napachukia napaona ni kama kaburini.
“Nakuapia siwezi…siwezi…siwezi kabisa kurudi huko nyumbani hata kama nitaambiwa kupelekwa na majeshi yote ya hapa nchini ambayo huwa nayaona wakati wa sherehe mbalimbali za kitaifa hapa Dar es Salaam, nakwambia sirudi nyumbani, huko nilishasema kwamba nitarudi nikiwa marehemu sijitambui…nitapelekwa kuzikwa tu.’’
Hayo ni maneno ya mtoto Bibiana Mbushi (12) mwenye ulemavu wa ngozi (albino) akiwa na mdogo wake Tindi Mbushi (10) ambao kwa sasa wanaishi uhamishoni jijini Dar es Salaam baada ya kuchukuliwa na msamaria mwema ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, Al Shaymaa Kweigry.
Watoto hawa ni wazaliwa wa kijiji cha Nyamwilolelwa, kata ya Chigunga, tarafa ya Butundwe umbali wa zaidi ya kilomita 50 kutoka mjini Geita, ambako Bibiana alikatwa mguu wa kulia na vidole vitatu vya mkono wake wa kushoto kuondolewa vyote, ambapo wahujumu walitoweka na viungo vyake hivyo kwenda kusikojulikana na hadi sasa haijulikani vilikwenda wapi na kufanya kazi gani.
Hayo yalitokea mwendo wa saa sita usiku wakiwa wamelala nyumbani, ambapo kitendo hicho
kilifanywa huku mdogo wake, Tindi akishuhudia kwa macho yake. Hakika inaumiza ukipata
simulizi ya namna ambavyo Bibiana alivamiwa akiwa yeye na wenzake watatu ndani ya nyumba usiku huo, hasa kwa maumivu aliyopata.
Mwaka wa tatu umepita sasa, Bibiana hana mguu wake wala vidole vitatu vya mkonowe,
vimechukuliwa na wasiojulikana kikatili na isijulikane kuvifanyia kazi gani.
Bibiana anasema ni siku ambayo ni vigumu sana kuisahau katika maisha yake huku akibainisha kwamba ni tukio ambalo litabaki kuwa simulizi katika maisha yake yote, isipokuwa anamshukuru Mungu kwa kumweka hai hadi sasa.
“Unyama niliofanyiwa ni mkubwa na kuna wakati napata shida hata kuwasimulia watu ambao
wamekuwa wakiniona na kuniuliza kilichonisibu hadi kufikia hatua ya kukosa mguu na kuwekewa mguu bandia, kuna wakati nimekuwa nikifikiria kusema uongo kwa wale wanaoniuliza lakini napata tena wasiwasi kwamba uongo ni dhambi inanilazimu kusema tu ukweli.
“Lakini nataka niseme jambo moja na kuliweka wazi kabisa kwamba malipo ni hapa hapa
duniani…naamini kwamba ipo siku moja Mwenyezi Mungu atafunua mambo na kuweka kila kitu wazi…lakini nawaombea sana Mungu awalinde na kuwaweka hai walionifanyia kitendo hiki,’’ anasema mtoto Bibiana kwa imani.
Bibiana na mdogowe Tindi wanasoma Kongowe Adventist Academy iliyoko Kibaha, mkoani
Pwani ambapo mwaka huu wanaingia darasa la tatu. Hafurahii kuishi mbali na wazazi wake, lakini mazingira ya wakatili waliokata mguu wake yanamlazimu.
“Sifurahii kutengana na wazazi wangu, si kwamba labda kwa sababu haya maisha ninayoishi
huku ni mazuri sana ukilinganisha na yale ya kule kijijini kwetu…la hasha…ni kwa sababu tu ya unyama niliofanyiwa siku ile tulipovamiwa ndiyo maana nimetokea kupachukia nyumbani kwetu.
“Kuna wakati huwa nawakumbuka ndugu zangu hadi nafikia hatua ya kuangua kilio hata kama
nipo darasani…lakini kwa sababu tu siwezi kwenda nyumbani kwetu kwa hofu ya kuuawa na wale watu waliokuja kunikata mguu na vidole inanilazimu nikae huku huku,’’ anasema Bibiana.
Watoto hawa walichukuliwa na Shaymaa ambaye pia ni albino baada ya HABARILEO kuandika
habari mbalimbali na makala zilizohusu maisha ya watoto hao katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, baada ya kukumbwa na mkasa huo. Walilazwa kwa ajili ya matibabu kwa miezi mitatu.
Tindi ambaye pia ni albino hakujeruhiwa, lakini alilala kitanda kimoja na dada yake hadi alipopona. Baada ya Bibiana kupona walikataa katakata kurejea nyumbani kwao kijijini, kwa hofu ya kuuawa na wahujumu wale au wengine ambao walikithiri kusaka viungo vya albino au kuwaua.
Hawakuwa tayari kwenda mahali popote, isipokuwa wanahitaji kuishi hapo hapo hospitalini. Tindi ndiye aliyeonekana kuwa mwoga zaidi. Hasa alikuwa akimwogopa kila mtu aliyemwona isipokuwa muuguzi aliyekuwa akiwahudumia na mwandishi wa makala haya ambaye tangu siku ya kwanza alikuwa akienda kuwashuhudia hospitalini hapo hadi walipopona.
Woga wa Tindi unatokana na alivyoshuhudia majambazi wakimkata mguu dada yake hadi kufikia hatua ya kuunyofoa na kuondoka nao. Anasema ilimlazimu kushuhudia tukio hilo mwanzo mpaka mwisho bila hata chembe ya kelele kwa hofu ya kwamba huenda wangemtenda
vile na yeye.
“Kile kitendo nilikishuhudia mwanzo hadi mwisho kwa macho yangu haya, iliniumiza sana kwa sababu aliyekuwa anafanya kile kitendo alikuwa ni mtu mwenye rangi nyeusi si kama hii yangu… ndiyo maana siwapendi watu wa aina hiyo na nawaogopa sana, hasa wanaume, kidogo wanawake tunakaa na kuongea nao,’’ anasema Tindi.
Shaymaa alijitokeza na kuwafuata mwezi mmoja baada ya watoto hao kupona, akafuata taratibu za kuwachukua kwenda kuishi nao. Hata hivyo naye pia alikumbana na kasheshe kubwa baada ya kukataliwa kwa dakika kadhaa na albino hao hadi walipobembelezwa na mwandishi wa makala haya pamoja na muuguzi aliyekuwa akiwalea hospitalini hapo.
Bibiana anasema ndoto zake ni kuja kufanya kazi benki na hasa kuwa gavana wa Benki Kuu (BoT), hali inayomfanya kuwa na jitihada kubwa katika kusoma, kiasi cha kushika nafasi ya tatu kati ya watoto zaidi ya 190 darasani.
Mdogowe anasema ndoto yake ni kuwa mbunge au askari polisi. “Nikifanikiwa kuwa mbunge…kama mama yangu hapa (Shaymaa) ili niwasaidie watu mbalimbali walio na shida
itakuwa sawa…lakini nitapenda zaidi kuwa askari polisi.
Lengo langu hapa ni kuhakikisha nakuja kuwakamata watu wote waliomkata dada yangu mguu,’’ anasema Tindi kwa msisitizo. Kabla ya kwenda Dar es Salaam, Bibiana na Tindi walichukuliwa na kupelekwa katika shule ya St. Mary’s jijini Mwanza na kusoma kwa muhula mmoja, ndipo Shaymaa aliamua kuwahamishia katika shule nyingine.
Shaymaa anasema lengo la kuwahamishia ni umbali uliopo kati ya Mwanza na Dar es Salaam, umbali uliokuwa ukimpa wakati mgumu kwenda kuwaona, hasa wanapougua na pia nyakati za kufungua na kufunga shule.
“Unajua Mwanza hadi Dar es Salaam kuna umbali mrefu sana; nilikuwa nikipata shida sana kwenda na kurudi au kuwasafirisha wao, na safari zao zilikuwa ni kwa ndege si basi, kwa hiyo utaona ni namna gani kulikuwa na kazi kubwa ndiyo maana nikaamua kuwahamishia Dar es Salaam ambako ni karibu hata pakijitokeza tatizo lolote ni rahisi kufika mara moja na kuwaona.
“Binafsi nafurahi kuishi nao kwa sababu kwanza ni waelewa sana watoto hawa na wamenipa ushirikiano wa kutosha, ndiyo maana unaona wanaishi hapa nyumbani kwetu na hawa ndugu zangu nao wanawapenda sana.
Kwa ujumla maisha yao ni mazuri na mimi wananitia moyo kwa sababu hata maendeleo yao ya
shule ni mazuri sana,’’ anasema Shaymaa.
Mbunge huyo ana mpango wa kuhakikisha watoto hao wanaishi vizuri na kupata elimu bora ili jamii itambue kwamba albino ni sawa na watu wengine wa kawaida wenye ngozi nyeusi, tofauti na ilivyo sasa ambapo wamekuwa wakionekana kama si binadamu wa kawaida.
“Nataka wasome ili jamii itambue kwamba hata watu wenye ulemavu wa ngozi kama sisi tukiwezeshwa tunaweza, lakini kubwa nataka siku moja nao waweze kusaidia familia yao iliyo kijijini kwao,’ ’anasema Shaymaa.
Kutokana na Bibiana na Tindi kukataa kurudi nyumbani kwao hata kuwasalimia ndugu zao, ndugu zao husafiri kutoka kijijini hadi Dar es Salaam kuwaona watoto hao.
Chanzo:HabariLeo
No comments:
Post a Comment