ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 7, 2011

Kama umeshtukia ni mbabaishaji, kwanini umng’ang’anie?

Assalam alaikum mpenzi msomaji wangu wa safu hii. Ni matumaini yangu kwamba kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu u bukheri wa afya na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku hasa katika kuyatimiza yale ambayo umepanga kuyafanya mwaka huu wa 2011.


Mpenzi msomaji wangu, asilimia kubwa ya watu wako kwenye ulingo wa mapenzi. Wapo walio katika ndoa, wapo walio katika uchumba na kuna wale wenzangu na mimi ambao bado wapo kwenye urafiki wa kawaida.

Niliodhamiria kuwazungumzia wiki hii ni wale walio na wapenzi wababaishaji ambao wapo katika penzi lisilokuwa na nyuma wala mbele. Yaani mtu anakuwa na mpenzi wake kwa muda mrefu lakini hawana malengo yoyote zaidi ya kuliendesha penzi kisanii huku siku zikisogea.

Huwa najiuliza, ni kupendana kwa aina gani huko ambako watu wanakaa kwa muda mrefu lakini hata siku moja hawajawahi kuzungumzia suala la kuja kuishi pamoja kama mke na mume?

Inaniuma sana pale ninapowaona baadhi ya wasichana ‘wakizinguliwa’ na wapenzi wao, yaani hawana sauti ya kuhoji juu ya hatma ya maisha yao hali inayoashiria kuwa, hawako na watu sahihi.

Sasa kwanini wewe msichana usiwe na msimamo na maisha yako? Kwanini ukubali kuburuzwa wakati wewe pia una haki ya kujua mustakabali wa maisha yako ya baadaye? Au hutaki kuipata ile heshima ya kuwa mke wa fulani?

Mimi nadhani ni vyema ukamweleza kabisa huyo mpenzi wako kwamba, sawa anakupenda lakini huu siyo wakati wa kuchezeana na kuachana, ana malengo gani ya baadaye na wewe? Ukiona anajiumauma na kutokupa majibu ya msingi, huna sababu ya kuendelea kuwa naye bali muache na uangalie utaratibu mwingine.

Tatizo walilonalo wasichana wengi ni kushindwa kujizuia pale mmoja anapotokea kumzimia mwanaume fulani, yaani anakuwa hasikii la kuambiwa na yuko tayari kwa lolote kiasi cha kufikia hatua ya kuhatarisha maisha yake.

Sidhani kama una sababu ya kujishusha kiasi hicho, wewe ni mwanamke unayestahili kuwa na mwanaume ambaye baada ya kipindi fulani atasema maneno haya: “Nimekuwa na wewe kwa muda mrefu, nimekusoma tabia zako na nimegundua kuwa una kila kigezo cha kuwa mke wangu wa maisha.

Akishakutamkia maneno hayo, unakuwa na nguvu sasa ya kumpenda zaidi, kumthamini na kumfanyia kila kitu ambacho kitamfanya aamini kuwa amempata mwenza wa kweli. Kwa kufanya hivyo naamini penzi lenu litadumu na kujikuta mnatimiza ndoto zenu.

Mpenzi msomaji, mapenzi yamekuwa yakiwasumbua walio wengi katika maisha yao hadi wengine kufikia hatua ya kujilaumu kwanini wamewapenda walionao sasa.

Wapo ambao wamepoteza maisha yao kwasababu tu ya mapenzi, wapo waliochanganyikiwa, kuathirika kisaikolojia na wengine kuachishwa kazi kwasababu ya mapenzi. Kimsingi mapenzi ni hatari sana hasa pale unapojikuta umedondokea sehemu ambayo hukustahili.

Lakini sasa, licha ya mapenzi kuleta matatizo kwa binadamu bado tunaambiwa kwamba, utakuwa peke yako kwa muda fulani tu wa maisha yako lakini mwishowe utalazimika kutafuta mwenza ambaye utaishi naye katika maisha ya mume na mke.

Suala la kujiuliza ni kwamba, kama huyo unayempenda haonyeshi dalili za kuja kukuoa, kuna ulazima wa kuendelea kung’ang’ania penzi lake? Mimi nasema, hakuna ulazima wa kuendelea kuwa naye bali unatakiwa kumuacha na kuangalia maisha yako. Kamwe usikubali kuwa mtumwa wa mapenzi. Usikubali kulia kila siku kisa mwanaume.

Nalazimika kusema hivyo kwasababu, mapenzi ya sasa yamejaa usanii wa hali ya juu kiasi kwamba ukifanya uchunguzi wa haraka haraka utabaini kuwa, wengi wanachezeana tu.

Si ajabu huyo uliyenaye anaonesha kukupenda kwa dhati lakini amini usiamini inawezekana ni gelesha tu na wala hana nia nzuri na wewe.

Ndiyo maana inashauriwa unapotokea kumpenda mtu fulani na yeye akakutamkia kwamba anakupenda, kuwa na imani ana penzi la dhati kwako kisha endelea kufanya utafiti katika kila analolifanya. Ukiwa mjanja utabaini kama umepata au umepatikana.

Ni hayo tu kwa leo, tuonane tena wiki ijayo kwa mada nyingine kali zaidi...

No comments: