![]() | |
| |
|
"TUNAJUA matokeo yetu yamewanyong'onyesha Watanzania, hatutawaangusha tena,
tutaifunga Uganda na kufuzu nusu fainai," hiyo ni kauli ya nahodha wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa akizungumzia mchezo wa leo.
Leo timu ya soka ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' itashuka kwenye Uwanja wa Polisi mjini hapa kuanzia saa 8:45 za huku sawa na saa 9:45 za Afrika Mashariki kumenyana na Uganda 'The Cranes' mchezo wa mwisho wa michuano ya soka Nchi za Bonde la Mto Nile hatua ya makundi.
Ni mchezo ambao lugha inayotakiwa kwa Stars ni ushindi wakati The Cranes wimbo wao ni 'hata sare' watakuwa wamefuzu nusu fainali.
Kikosi cha Uganda kilichopo mjini hapa hakina nyota wengi waliokuwa Dar es Salaam mwezi uliopita kwenye michuano ya Chalenji, badala yake wachezaji walio wengi ni chipukizi, lakini walio na uwezo mkubwa wa kusakata soka.
Uganda iliwaduwaza mashabiki wa Misri Jumamosi baada ya kuibana vilivyo Misri 'Farao' karibu dakika 89 za mchezo na kufungwa bao pekee dakika ya 90 mfungaji akiwa Ahmed Hassan Gedo.
Hali hiyo imeifanya Uganda sasa kuwa midomoni mwa wadau wa soka mjini hapa kwamba ni timu nzuri na inapewa nafasi kubwa ya kuifunga Stars leo.
Tayari watabiri wameanza kupanga nusu fainali itakavyokuwa kwamba Misri itacheza na Kenya ambayo itashika nafasi ya pili Kundi B, kisha Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo 'DRC' itakayoongoza Kundi B itacheza na Uganda itakayoshika nafasi ya pili Kundi A.
Hayo ni matarajio ya mashabiki wengi hapa. Lakini Nsajigwa na wenzake wanasema
watawashangaza wengi na hawaoni kwa nini wasiingie nusu fainali, hivyo kazi yao leo ni moja kumpiga Mganda, kwani nia wanayo, uwezo wanao na sababu pia wanayo.
"Tumedhalilika mechi mbili zilizopita, Uganda itakuwa chakula yetu," alisema Nsajigwa, kauli
pia iliyozungumzwa na Mrisho Ngasa, Jerry Tegete ambao wameahidi kuonesha cheche zao leo wakipata nafasi ya kucheza.
Kocha wa Taifa Stars, Jan Poulsen alisema anatarajia mechi itakuwa ngumu, lakini kwa vile wanaingia wakiwa wanajua makosa halitawasumbua sana.
Alisema amewapa maelekezo ya kutosha washambuliaji wake, pia sehemu ya ulinzi na ana hakika watafanya kile alichowaelekeza kuhakikisha wanapata ushindi mnono.
Kwa upande wake kocha wa Uganda Bobby Williamson naye alisema mechi itakuwa ngumu, lakini ameshajua udhaifu wa Stars itakuwa si kazi ngumu kushinda.
Misri inayoongoza Kundi A ikiwa na pointi sita tayari imetinga nusu fainali na leo inamaliza na Burundi mchezo utakaofanyika mjini Ismailia, ambapo hata kama itafungwa haitaathirika.
Lakini ili Stars ifuzu nusu fainali itabidi iifunge Uganda leo, kisha iombee Misri iifunge Burundi ama itoke nayo sare, vinginevyo kama Burundi itashinda basi itabidi utazamwe uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Mpaka sasa Stars imefungwa mabao sita na imefunga mawili, hivyo ina deni la mabao manne, wakati Burundi imefungwa manne na imefunga mawili huku nayo ikiwa na deni la mabao mawili.
Uganda ni ya pili ikiwa na pointi tatu na mabao manne ya kufunga, ikiwa imefungwa mawili, huku Burundi ikiwa ya tatu na Stars ya mwisho. Zote zina pointi moja.
Kundi B leo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), inacheza na Sudani ambayo mchezo wa kwanza ilifungwa bao 1-0 na Kenya kabla ya DRC kuifunga Kenya bao 1-0, hivyo mchezo huo utaamua timu za kufuzu nusu fainali, ingawa DRC ina nafasi kubwa kwani hata sare itakuwa imefuzu.
Michuano hiyo inashirikisha nchi saba zilizogawanywa makundi mawili na timu mbili za juu kila kundi zitacheza nusu fainali, wakati zilizoshika nafasi ya tatu zitacheza kuwania mshindi wa tano.
chanzo:Habari Leo

No comments:
Post a Comment