Jackson Odoyo,ZanzibarSHEREHE za miaka 47 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zitaitimishwa leo kwa aina yake wakati Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein atakapokuwa akishuhudia watani wa jadi Simba na Yanga wakionyeshana ubabe kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa majira ya Saa 2:30.
Ugeni huo wa Rais Shein ndio uliosababisha kubadilisha ratiba ya mechi hiyo kutoka saa 10:30 jioni hadi saa mbili usiku kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa mashindano hayo Mohamed Raza.
“Tumelazimika kubadilisha ratiba ya mechi hiyo baada ya kumuomba Dk Shein kuwa mgeni rasmi naye kukubali, lakini akaomba yafanyike marekebisho kidogo ya ratiba hiyo kutokana na majukumu yake, ”alisema Raza.
Alisema kamati yake imefurahishwa na hatua ya Rais Shein kukubaliana na ombi lao kwa hiyo wao kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama watahakikisha mambo yote yanakwenda kama yalivyopangwa.
Miamba hiyo inashuka kwenye uwanja wa Amaan huku vikosi vyao vikiandamwa na majeruhi kibao pamoja na mapengo ya wachezaji tegemeo waliopo timu ya Taifa.
Simba inaingia katika fainali hizo ikiwa na majeruhi wanne ambao ni Mohamed Banka, Emanuel Okwi, Salum Kanoni na kipa Ally Mustafa, huku wapinzani wao Yanga huenda ikiwakosa Chacha Marwa, Ernest Boakye,Yew Berko pamoja na Iddy Mbaga kutokana na kuwa majeruhi.
Akizungumza na Mwananchi jana mjini hapa kocha wa Simba, Patrick Phiri alisema mechi hiyo itakuwa ngumu kuliko alivyokuwa akitarajia ingawa tangu awali alikuwa na hamu ya kukutana na Yanga katika hatua ya nusu fainali.
“Timu yangu inakabiriwa na majeruhi wanne ambao ni Okwi, Kanoni, Banka pamoja na Mustafa, huku wachezaji wengine wakiwa Misri, lakini sijakata tamaa kwa sababu bado ninaangalia hali za majeruhi hao mpaka kufikia kesho mchana," alisema Phiri.
Wakati Phiri akilia na majeruhi kilio hicho pia kimemkumba kocha wa Yanga, Kostadin Papic ambaye analalamika kuwa na majeruhi Marwa, Boakye, Berko pamoja na Mbaga, lakini anasubiri kauli ya daktari kuona kama ataweza kuwatumia.
“Mechi itakuwa ngumu sana hasa kwa upande wangu kwa sababu nina majeruhi katika timu huku wachezaji wengine wakiwa na timu ya taifa,” alisema Papic.
ULINZI
Homa ya pambano hilo imepanda hali iliyosababisha kuongezeka kwa ulinzi kwenye kambi ya timu hizo.
Simba iliyoweka kambi katika maeneo ya Mbweni nje kidogo ya kisiwa cha Unguja imeongeza ulinzi katika kambi hiyo na kuzuia watu wasiojulikana kuingia kwenye kambi hiyo.
Hali kama hiyo pia imejitokeza katika kambi ya Yanga ambayo iko katika hotel ya Al Anoor iliyopo katikati ya mji wa Unguja, kambi hiyo imewekewa ulinzi mkali huku kila mchezaji akipigwa marufuku kutoka nje ya hoteli hiyo.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wachezaji hao walisema hali ya ulinzi katika kambi zao si ya kawaida.
“Ebwanaee si unajua mechi za Simba na Yanga wakubwa wanavyokuwa na imani tofauti hapa kambini haruhusiwi mtu kuja, kuna ulinzi mkali hakuna anayeruhusiwa hata kutoka nje ya geti,” alisema mchezaji mmoja wa Simba huku akiomba jina lake lisiandikwe gazetini.
“Hali si shwari katika kambi hii sijawahi kuona mchezaji akipewa ulinzi, hii ni mara yangu ya kwanza, hata Mwanza haikuwa hivi hii imezidi kipimo, yaani hapa ukitoka nje ni wakati wa chakula na kurudi ndani,”alisema kinda wa Yanga kwa masharti ya jina lake kutoandikwa gazetini.
Naye msemaji wa timu ya Yanga, Luis Sendeu alisema ulinzi umezidi kuimarishwa katika kambi hiyo na kwamba kila kitu kilibadilishwa haraka tangu timu ilipoingia fainali.
“Kaka hapa hali ni ulinzi tu si unajua mechi za Simba na Yanga ilivyo na vibweka vingi hivyo ni lazima tuzidishe ulinzi,”alisema Sendeu.
VIINGILIO
Viingilio vya mchezo huo vitakuwa Sh 10,000 badala ya Sh5,000 kwa jukwaa kuu ama VIP kuu na Sh 5,000 badala ya Sh 3,000 kwa majukwaa ya pembeni, huku jukwaa la Urusi likiwa ni Sh 3,000 badala ya 2,000.
Akizungumza mjini hapa Mwenyekiti wa kamati ya mashindano, Mohamed Raza alisema wamelazimika kupandisha viingilio hivyo kutokana na umuhimu wa mechi hiyo.
“Viingilio vimepanda kidogo ukilinganisha na vingilio vya zamani na tuna imani mashabiki wa soka katika visiwa hivi wataweza kuvimudu,”alisema Raza.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment