ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 12, 2011

Zanzibar; Mapinduzi Day, January 12, 1989!


Leo Jumatano, Januari 12 ni Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar. Shuleni nilipenda sana kusoma habari za Wanamapinduzi wa dunia hii. Kusoma habari za mapinduzi ya umma katika sehemu za dunia. Habari za Mapinduzi ya Zanzibar zilinivutia sana. Nilipata kusoma kitabu cha John Okello kilichonivutia sana kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar. 


Kupitia historia hiyo nilifahamu habari za wanamapinduzi kama vile Abdulahman Babu, Kissasy na wengineo. Nilipomaliza Form Four pale Tambaza Secondary nilibahatika kufanya safari ya kwanza maishani mwangu kuvuka bahari. Safari ya kwenda Unguja.
Huko nilikuwapo wakati wa sherehe za Mapinduzi Jan 12, 1989. Nilifurahia kuwapo mahala palipokuwa na vuguvugu la Mapinduzi ya mwaka 1964. Kuviona kwa macho na kutembea kwenye vitongoji vya Zanzibar; Mkunazini, Mji Mkongwe na kwengineko. 

Nakumbuka shuleni tulisoma kuwa Karume alikuwa kiongozi wa Mapinduzi yale. Taarifa hizi si sahihi ukisoma maelezo kwenye kitabu cha John Okello na hata mwandishi mahiri Ryszard Kapuchinski. Mwandishi huyu alikuwapo Dar na Zanzibar wakati wa mapinduzi. Kapuchinski anaandika; kuwa Karume alikuwa Dar wakati mapinduzi yale yakiendelea. Kapuchinski anamzungumzia Karume kama mtu aliyekuwa akiongea kwa sauti ya juu sana hata ukikaa nae karibu. Mara nyingi Karume alikuwapo pale New Africa Hotel walipokutana wanamapinduzi wengi wa bara hili.

Naam. Tukirudi kwenye safari yangu ya kwanza kwenda Unguja, basi, wakati huo safari yangu ya kwenda Unguja ilinichukua zaidi ya saa saba. Bandarini Dar kulikuwa na vyombo kama MV. Zainab, Ashura na vinginevyo. Nilisafiri na chombo kidogo kiitwacho Ras Nungwi ( Kilizama miaka ya 90). Nakumbuka Ras Nungwi ilijaza shehena kubwa ya mizigo. Kabla ya kuingia bandarini Zanzibar nahodha alituomba abiria tuliosimama mbele tuiname ili aone vema. Hakuwa na chombo cha kumpa mwelekeo sahihi. Leo unakwenda Zanzibar kwa saa moja! Naam. Tumetoka mbali.


                                      CHANZO:http://mjengwa.blogspot.com/

No comments: