POLISI mkoani Tabora, inamsaka Amos Gambo mkazi wa kijiji cha Mtakuja Manispaa ya Tabora kwa tuhuma za kumbaka bintiye wa kufikia mwenye umri wa miaka nane ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Mtakuja.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Liberatus Barlow, alidai tukio hilo limetokea saa saba na nusu usiku, wakati mama wa mtoto huyo alipokuwa ameenda msibani.
Alidai mama wa mtoto huyo, Lucia Mbulwa, aliondoka kwenda kulala msibani kwa jirani na kuwaacha watoto pamoja na mzazi huyo wa kiume ambaye hata hivyo badala ya kuwalinda kama ilivyo kawaida, aliamua kumdhuru mmoja wao.
Kwa mujibu wa madai hayo, Gambo alitoweka nyumbani mara baada ya kufanya uhalifu huo na asubuhi mama huyo aliporejea alikuta binti huyo akiwa katika hali mbaya.
Alidai mama huyo alimfanyia uchunguzi wa haraka haraka ambao ulimuwezesha kutambua mtoto huyo wa kike alikuwa amebakwa na baba yake huyo.
Lucia wakati akiolewa na Gambo tayari alikuwa na mtoto mmoja ambaye alienda naye kwa mumewe kwa ajili ya kumlea.
Alisema mama huyo alipiga kelele zilizowafanya majirani na ndugu zake kufika nyumbani hapo na kushuhudia madhara aliyoyapata mtoto huyo baada ya kufanyiwa kitendo hicho cha kinyama.
Mtoto huyo alikimbizwa Polisi na baadaye hospitalini kwa ajili ya matibabu na hali yake bado ni mbaya.
Kamanda Barlow, alitoa mwito kwa watu wote wanaomtambua Gambo, wawasiliane na Polisi mara moja ili kuwezesha mtuhumiwa kukamatwa na kufikishwa katika mikono ya sheria.
No comments:
Post a Comment