
Kocha wa timu ya Simba,Patrick Phiri
Yanga inapambana na Dedebit ya Ethiopia katika mchezo wa pili wa raundi ya awali baada ya kwenda sare ya 4-4 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.
Wawakilishi wengine wa Tanzania, Simba watakuwa kwenye Uwanja wa Uhuru kesho kurudiana na Elan ya Comoro katika mfululuzo wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba inaingia kwenye uwanja huo ikiwa na kila sababu ya kushinda baada ya kwenda suluhu na mabigwa hao wasiofahamika sana kwa soka kutoka Comoro.
Yanga ambayo kwa muda mrefu imezongwa na bundi wa migogoro, wanaingia kwenye mapambano huo wakitafuta ushindi, kwani sare ya aina yoyote itakuwa imewatupa nje ya michuano hiyo.
Kwa kuwa dunia ni kijiji, tunaimani salaam zetu zitawafikia wachezaji wa Yanga, tunawasihi kufanya kile kilichowapeleka badala ya kufikiria kuumizwa na mapokezi mabaya ya wenyeji wao, Ethiopia. Ushindi ni lazima ili kutoa aibu ya Tanzania kuishia raundi ya awali.
Wiki mbili zilizopita, tulishangaa kuona Simba wanaishangilia Dedebit ilhali viongozi walishakubaliana kutoangushana na kupeana nguvu katika mashindano ya kimataifa. Mashabiki wa Simba na Yanga wanatakiwa kubadilika.
Baada ya viongozi wa pande zote (Simba na Yanga) kukubaliana kushirikiana katika michuano ya kimataifa, ni wazi uwanja mzima unatakiwa kushangilia bila kujali upande kwa kuwa wanaocheza si Simba ama Yanga, ni kwamba wanaiwakilisha Tanzania.
Kama tulivyosema hapo juu, japokuwa Yanga iko ugenini nchini Ethiopia, hatutarajii kuona ikitolewa katika hatua hii, kwa kuwa wamefahamu aina ya soka ya wapinzani wao na tunaamini wamejiandaa kikamilifu kwa kurekebisha kasoro zilizojitokeza mchezo wa kwanza.
Simba kwa upande wao, wafahamu, wako nyumbani na siku zote uwanja wa nyumbani ni msingi wa kujiamini na inatakiwa kutumiwa kikamilifu kupata ushindi.
Wekundu hao wa Msimbazi, wana kila sababu ya kushinda mechi kwenye uwanja wa waliouzoea. Wakati mwingine inakuwa tabu sana kwa timu kucheza nje ya dimba wasilolizoea wakashinda. Simba pia wanacheza katika hali ya hewa waliyoizoea na ni wazi haitowasumbua.
Kwa upande mwingine, mashabiki wa soka na Watanzania kwa ujumla ni wakati wa kuwaombea kila la kheri wachezaji na viongozi wa Simba, Yanga pamoja na kuziombea dua timu nyingine za Tanzania katika michuano hiyo.
Timu za KMKM ya Zanzibar iliyokuwa icheze na DC Motema Pembe mjini Kinshasa, na Zanzibar Ocean View iliyokuwa iende huko dhidi ya AS Vita, mechi zake zimeahirishwa kwa sababu mbalimbali.
Tunawatakia kila la kheri wachezaji na makocha ambao ndiyo mabalozi wetu katika mashindano hayo makubwa kwa klabu Afrika. Cha msingi ni kushinda katika mechi hizi za marudiano za raundi ya awali na kuondokana na aibu kutolewa mapema katika raundi hiyo.
Mungu wabariki wawakilishi wetu wafanye vizuri na kuiletea sifa Tanzania. Mungu ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment