ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 12, 2011

Watatu washikiliwa sakata la vichanga Mwananyamala


Tume iliyoundwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, kuchunguza sakata la kufukiwa vichanga kumi katika shimo moja, imetoa ripoti yake ambayo imesema watumishi watatu akiwemo mlinzi wa hospitali ya Mwananyamala walishiriki katika sakata hilo.
Ripoti hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wake, Dk. Charles Karumbo, akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana na Mstahiki Meya Yusuph Mwenda, Mkurugenzi wake Raphael Ndunguru pamoja na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela.

Akisoma matokeo ya uchunguzi wa tume, Dk Karumbo alisema vichanga hivyo 10 vilikutwa katika shimo moja eneo la Mwananyamala Januari 31 Mwaka huu, walitokea katika Chumba cha Kuhifadhia Maiti cha Hospitali ya Mwananyamala,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa, Raphael Ndunguru alisema kwamba watumishi waliopatikana kuhusika na sakata hilo wameshachukuliwa hatua za awali za kiutawala. Lakini hatua kamili zitachukuliwa kutegemaeana na hatima ya upelelezi wa kesi hiyo.
Aliwataja watumishi waliobainishwa na Tume kushiriki katika kadhia hiyo kuwa ni Said Ally Salum, msimamizi wa chumba cha maiti, Siraji Ally Mbuli, msaidizi wa chumba hicho pamoja na Sophia Hassan Abdallah (Kandoro) ambaye ni mlinzi hospitalini hapo.
Kwa upande wake, Kamanda Kenyela alithibitisha polisi kuwashikiria watuhumiwa na bado wanamtafuta James Ngobile anayetuhumiwa kuwachukua na kuwafukia vichanga hivyo. Aidha alisema bado wanaendelea kuwatafuta wazazi wa vichanga hivyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: