Wakili Michael Ngallo amewasilisha maombi mahakamani ya kukata rufaa Mahakama Kuu kuomba mapitio ya uamuzi wa kuvifuta vielelezo vinavyothibitisha Yusuf Manji ni fisadi papa.
Aidha, Ngallo alidai kuwa hakushangazwa na uamuzi huo uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kutokana na mahakama hiyo kutupilia mbali kila anapowasilisha maombi wakati wa usilikilizwaji wa kesi hiyo.
Manji amefungua madai ya fidia ya Shilingi Moja dhidi ya Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, kwa madai kuwa alimkashifu kwa kumuita ni fisadi papa.
Ngallo alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana, baada ya kutolewa uamuzi wa kuvikataa vielelezo hivyo, kwa maana hiyo hakuridhika na uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo.
“Nilitegema mahakama kutoa uamuzi huu, lakini sijaridhika nao kwa sababu utasababisha Mwenyekiti wa IPP, kushindwa kuvitumia vielelezo kwenye kesi hii. Hata hivyo, uamuzi huo hauwezi kuzuia mteja wangu kwenda Mahakama Kuu, kuomba mapitio ya kesi hii,” alidai.
Aliongeza kuwa kuvifuta vielelezo hivyo ni sawa na kumfunga mteja wake dhidi madai yaliyopo mahakamani dhidi yake.
Hata hivyo, wakili Richard Rweyongeza wa Manji, alidai mahakama imetoa uamuzi sahihi na kwamba madai ya Ngallo hayana msingi yatupiliwe mbali.
Hakimu Katemana alisema atatoa uamuzi ama wa kuhamishia shauri hilo Mahakama Kuu kwa ajili ya mapitio au la, Jumanne ijayo.
Awali, mawakili wa Manji, waliomba mahakama kuondoa baadhi ya vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo kama ushahidi na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, kikiwemo cha kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd kuhusishwa na mteja wao.
Mengi aliwasilisha vielelezo 14 vya ushahidi kikiwemo cha Manji kuhusishwa na kampuni ya Kagoda ambayo ilitajwa kuwa ilihusika katika uchotaji wa mabilioni ya fedha kutoka Benki Kuu Tanzania (BoT).
Katika ushahidi wake, Manji alidai Aprili 23-27 mwaka 2009, Mengi kwa kutumia kituo cha televisheni cha ITV, alitoa madai kuwa Manji na wafanyabiashara wengine kuwa ni mafisadi papa, wanahamisha rasilimali za taifa kupeleka nje ya nchi na kwamba wameshiriki kikamilifu katika ufisadi wa ununuzi wa magari ya JWTZ, rada, mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma, mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSPF na NSSF, Dowans na Richmond.
Manji alifungua kesi ya madai ya kashfa dhidi ya Mengi na kituo cha televisheni cha ITV mwaka juzi akitaka amlipe fidia ya Sh. moja kwa madai kuwa alitumia televisheni yake kumkashifu kwa kumuita ‘fisadi papa’ na mmoja wa watu wanaopora rasilimali za taifa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment