ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 11, 2011

Lijue penzi la kweli-GPL

KWA mapenzi makubwa ya Allah Subhana Wataala, mu wazima wa afya, kama kuna wagonjwa basi Mungu awape neema ili waweze kupona upesi. Nina imani muda huu umeshikilia gazeti lako ulipendalo la Championi Ijumaa na macho yako yapo kwenye kona yako ya Mapenzi na Uhusiano, shukrani sana kwa hilo.

Najua una hamu kujua leo kiporo chetu kipo kwenye hali gani, kama kinalika au kimechacha? La hasha bado kipo salama kina moto wake ule ule, weka sahani ili nikupakulie.


Nitakuwa mwizi wa shukrani ikiwa nitashindwa kufikisha shukrani zangu kwa wote waliochangia mada zangu kila wiki. Kwa njia moja au nyingine wote wakiwa katika kupongeza, kushauri hata kukosoa ili kuhakikisha kona yetu inazidi kupanda chati kila kukicha kwa njia ya ujumbe ufupi au kwa kupiga simu kabisa.

Wapo waliotaka kujua na wale wapenzi ambao huwa kero kwenye nyumba, wapo kundi gani? Kwa vile mada hii ni ndefu kila kitu utakipata kuwa mfuatiliaji mzuri.

Bila kupoteza wakati tunaendelea na mada yetu, sehemu tuliyoiacha wiki iliyopita ‘Kwa nini umeachwa bila sababu maalum’. Haya tena leo tunaendelea tulipoachia pale nilipoongelea kanuni za mapenzi ili likikutokea ujue mpenzio amesimama upande gani.

Kwanza hebu tuyaangalie haya mafungu katika mapenzi ambayo ndiyo yaliyobeba mapenzi yetu ya kila siku. Hata kutoa majibu ya maswali uliyokuwa ukijiuliza.
Makundi ya mapenzi yapo kama ifuatayo;

• Penzi la kweli.
• Penzi la kudumu.
• Penzi la mpito.
• Penzi kwa ajili ya...
• Na penzi ambalo lipolipo tu na halimgharimu mtu wala kumpotezea muda.

Katika makundi haya yote, ndipo kuna vitu viwili upendo na tamaa, ambavyo ndivyo vilivyobeba makundi haya. Sasa twende pamoja ili tujue kila kundi linatabia gani?

Penzi la kweli:
Penzi la kweli lina upendo wa dhati ulio ndani ya wapenzi wawili, penzi hili limejaa huruma kwa wapendanao, kutokuwa tayari kumuona mwenzake aliteseka au kukosa raha kwa ajili yake.

Penzi la aina hii wapendanao mioyo yao hujaa woga kwa kuhakikisha wanakuwa watu wa furaha na utumia muda wao mwingi wakiwa pamoja kubuni mbinu kuhakikisha mwenza wake hajihisi upweke.

Watu wa kundi hili huwa wavumilivu kwa hali yoyote na ujitoa muhanga kwenye matatizo pia huogopa wao kuwa vyanzo vya matatizo. Huwasikiliza wapenzi wao kuliko mtu yeyote hata wazazi wao.

Hulifurahia penzi kuliko kitu chochote, hata kama hawana kitu wao upendo ni shibe ya mioyo yao. Ni wepesi kusamehe na kusahau maudhi kwa haraka hawapendi kujikumbusha maudhi yalioukeresha moyo wao. (Na mengine mengi yaliyobeba maana halisi ya mahaba)

Maelezo mengine ya makundi yanayofuata tukutane wiki ijayo ili ujue upo kundi gani au mpenzi wako yupo kundi lipi na kujua tabia ya kila kundi la mapenzi.

No comments: