ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 11, 2011

Tanzania yapeleka mjumbe kwa Gbagbo

Exuper Kachenje, Dodoma
TANZANIA imetuma ujumbe wake, nchini Ivory Coast kutafuta namna ya kusuluhisha mgogoro wa uongozi, kati ya Rais Laurent Gbagbo na hasimu wake, Alassane Ouatara.

Akizungumza na Mwananchi jana Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema  ujumbe huo ni wa mtaalamu na mwanadiplomasia, aliyemtaja kuwa ni balozi David Kapya.


Balozi Kapya aliyekuwa akimsaidia Rais mstaafu wa awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa katika kazi ya kutatua mgogoro wa Sudan ya Kusini, amekwenda Ivory Coast kuungana na wajumbe wa nchi za Afrika Kusini, Chad, Burkinafaso, Mauritania na Nigeria kushughulikia suala hilo.

Alisema balozi huyo, yupo Ivory Coast tangu Jumapili niliyopita na kazi kubwa aliyoifanya ni kufanya mahojiano na wadau wote wa mgogoro huo, na kwamba baadaye ataandaa ripoti.

AlisemaTanzania na nchi hizo, zipo katika kamati ya kutatua migogoro, barani Afrika na kwamba tayari wamekutana na kuwahoji wadau wote wa mgogoro huo.

Aliwataja wadau wa mgogoro huo, ambao wamehojiwa kuwa ni pamoja na Rais Gbagbo, Ouatara, tume huru ya Uchaguzi ya Ivory Coast (IEC), Kamati ya katiba (CC) na wananchi.

Alisema kazi iliyobaki kwa Balozi Kapya  ni kukabidhi ripoti yake kwa Rais Kikwete.

Alisema pia wajumbe wa nchi nyingine, watakabidhi ripoti zao kwa marais wa nchi zao, ili wazifanyie kazi na kuweka mikakati kabla ya marais hao, kukutana. 

"Ni kazi nzito, lakini naamini itafanikiwa, kesho Balozi Kapya na wale wengine watakwenda Addis Ababa kuandaa mazingira na baada ya hapo viongozi wakuu, watakutana," alisema Waziri Membe.

Alibainisha kuwa Rais Kikwete na marais wa nchi za Chad, Afrika Kusini, Mauritania, Burkinafaso na Nigeria watakutana katika mji Mkuu wa Mauritania Nouakchott ili kuweka mikakati kabla ya kukutana na Gbagbo na Quatara nchini Ivory Coast.

Membe alisema ni matumaini yake kuwa mgogoro wa Ivory Coast utamalizwa kwa busara za viongozi hao, ikiwemo Tanzania.


CHANZO:MWANANCHI

No comments: