ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 11, 2011

Waziri Nundu azomewa TRL

Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu
Pamela Chilongola na Juma Hamisi
WAZIRI wa Uchukuzi, Omar Nundu jana alizomewa na kundi la wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) ambao hawakuridhishwa na majibu ya Waziri huyo kuhusu madai ya stahili yao.

Kufuatia zomea zomea hiyo, mktano baina ya waziri huyo na wafanyakazi wa TRL ulivunjika hivyo Nundu aliondolewa haraka katika jengo la karakana ya reli jijini Dar es Salaam na watu waliodhaniwa kuwa ni maofisa wa usalama.

Wafanyakazi hao walionyesha kutoridhishwa na maelezo ya waziri huyo kuhusu hatua iliyofikiwa katika utatuzi wa kero zao mbalimbali ikiwa ni pamoja na mchakato wa kuvunjwa kwa mkataba wa uendeshaji wa reli ya kati, baina ya Serikali na kampuni ya Rites Consortium ya India.

Kabla ya kuvunjika kwa mkutano huo, Nundu alisema mchakato wa kuvunjwa kwa mkataba baina ya Serikali na Rites umekamilika isipokuwa unasubiri kusainiwa na pende husika.

“Hapa tulipofikia ni hatua ya kuachana na Rites, bado tu kusaini hiyo mikataba ya kusitisha, mpaka leo hii tumeulizia kwa hao wawekezaji kama kuna mkubwa anayeweza kusaini ili asaini na kusitisha mkataba kwa bahati mbaya hajapatikana,”alisema Nundu.

Kuhusu kiinua mgongo cha wafanyakazi hao, Nundu alisema serikali kwa sasa  haina fedha, hivyo kuwataka wawe wavumilivu.

Alisema hivi sasa wafanyakazi hao wanaweza kuendelea kuwasiliana na wanasheria wao kwa lengo la kubaini matakwa ya mikataba ambayo itasaidia kulipwa fedha hizo zitakapopatikana.

Alisema hivi sasa serikali inatafuta Sh 63 bilioni kwa ajili ya kufufua miundombinu ya shirika hilo na sio kuwalipa kiinua mgongo wafanyakazi.
“Hizo Sh 63 bilioni bado hazijapatikana ndio kwanza tunazitafuta ili kuboresha shirika la reli ambalo linayumba muda mrefu kama tutakubaliana tushirikiane kwa hilo ili kukuza uchumi wa nchi yetu,”alisema Nundu.
 
Kauli hiyo ndiyo iliyoonekana kuwachefua wafanyakazi hao wa TRL hivyo kuanza kumzomea wakisema kwamba hawataki siasa bali wanataka haki yao na kusisitiza kuwa walipwe kwanza kisha uboreshaji wa shirika hilo ufuate.

Wakati wakizomea, wafanyakazi hao walikuwa wameshika mabango huku wakiimba kwa kusema "fedha zetu, fedha zetu…. tumechoka na siasa zenu, amani ni tunda la haki bila haki hakuna amani, vitisho havitasaidia kutoa utatuzi wa matatizo yetu cha msingi utekelezaji.” 

 “Hamuwezi serikali mkaboresha vyuma hali binadamu tunaangamia kwa maisha magumu licha ya uzalendo tunaouonyesha hivyo hatuafiki kuboreshwa shirika hilo hali ya kuwa wafanyakazi tuna maisha magumu,” alisema mmoja wa wafanyakazi, Hassan Salim.

Salim alisema iwapo watalipwa mafao yao kazi itafanyika vizuri na hata wageni hawatahitajika tena kwenye shirika hilo.

“Kinyume na kulipwa mafao yatu ushirikiano na wawekezaji haupo na shirika litadhoofu na hatimaye kufa,”alisema Salim.

Naye mfanyakazi wa Karakana ya Morogoro, Kilia Nambita alisema wakati serikali inaingia mkataba na Rites, wafanyakazi hao waliweka wazi kwamba wawekezaji hao hawana uwezo wa kuendesha shirika hilo.

Alisema mpaka sasa shirika hilo halijafafanua fedha wanazozipata wanazipeleka wapi hivyo kuifanya serikali kuwalipa mishahara isiyokidhi.

Katibu Mkuu wa Chama cha wafanyakazi wa Reli (Trawu), Sylivester Rwegasira alisema walifichwa na serikali na kuambiwa kuwa mkataba huo ni siri na kuwataka wafanyakazi wawe na mshikamano.

“Matatizo haya yanasababishwa na serikali kutowasiliana na sisi katika suala zima la uendeshaji,”alisema Rwegasira.

Pia alisema mambo ambayo wameyalalamikia hayakujibiwa na Waziri hivyo makusudio yao ni kukutana leo na viongozi wa matawi yote ili kuzungumzia msimamo wao.

“Sisi tutakuna kesho (leo) na viongozi wa matawi yote kujadili suala hilo na kuweka msimamo wa kisha tutakuja kuwaeleze wenzetu nini hatua tutakazotakiwa kuchukua,”alisema Rwegasira.


CHANZO:MWANANCHI

No comments: