Advertisements

Tuesday, February 15, 2011

Maandamano Iran: Nini Kilichojiri-BBC

Baada ya maandamano mitaani nchini kote siku ya Jumatatu ,vyombo vya habari vya serikali na tovuti vimejaa maoni na mijadala kuhusu umuhimu wa matukio hayo.
Kwa viongozi wa upinzani wa vuguvugu la Green Movement, haya yalikuwa maandamano makubwa ya kuonyesha nguvu za wafuasi wao katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.
Lakini maoni ya mhariri wa gazeti lenye msimamo mkali Kayhan yaliwakebehi waaandamanji hao kuwa ni "genge la takataka" ambazo zinaweza kutupiliwa mbali.
Maandamano Iran

Ni wazi kabisa kuwa maandamano ya Jumatatu nchini Iran yaliishangaza serikali na viongozi wa upinzani wa vuguvugu la Green Movement.

Kwa vile watu walikuwa tayari kujitokeza mitaani bila kujali vikosi vya usalama kunaonyesha jinsi baadhi ya wananchi walivyo na hasira dhidi ya serikali.
Halikadhalika inabainisha kuwa madai ya serikali kuwa vuguvugu la Kijani limeishiwa hayana msingi.
Tangu kuzimwa kwa nguvu maandamano yaliyofuatia uchaguzi mkuu wa 2009 serikali imesisitiza kwamba hakuna vuguvugu lenye nguvu nchini Iran.
Wakati maandamano yakianza nchini kote siku ya Jumatatu na tovuti za upinzani zikivuma na taarifa kutoka mitaani -vyombo vya habari vya serikali viliendelea kuripoti kwamba hali ni tulivu.
Lakini wabunge wa Iran walipoanza kujadili matukio hayo katika bunge siku ya Jumanne,ilikuwa wazi kutokana na hasira zilizojitokeza katika mjadala huo kwamba wana wasiwasi mkubwa na kile kilichotokea.
Kwa mara ya kwanza kikao cha Majlis(bunge) kilisikia wito wa sio tu kuwafungulia mashtaka viongozi wakuu wawili wa upinzani - Mir Hossein Mousavi na Mehdi Karroubi - bali hata wauwawe. 
Ni vigumu kukisia watu wangapi walijiunga na maandamano mjini Tehran na miji mingine siku ya Jumatatu.
Sababu moja ni kwamba vikosi vya usalama vilifanya kila liliowezekana kuwazuia watu wasikusanyike katika eneo moja.
Wakiiga mfano wa maandamano katika uwanja wa Tahrir (Ukombozi) mjini Cairo, waandamanaji nchini Iran walielekea uwanja wa Azadi (Uhuru) mjini Tehran.
Lakini vikosi vya usalama vilizifunga barabara kuu zinazoelekea katika kitovu cha jiji ikimaanisha kuwa maandamano hayo yalitawanywa katika jiji zima.
Huu ndio mkakati uleule ambao watawala wamekuwa wakiutumia dhidi ya upinzani kwa jumla katika miaka miwili iliyopita.

Maandamano yasio na uongozi

Kwa kuwazuia viongozi wa vuguvugu la upinzani katika kifungo cha nyumbani na kuwatia mbaroni wengine wengi serikali imeweza kuwazuia wafuasi wa vuguvugu la Green, wengi wao wakiwa wa tabaka la katikati, kujaribu kuimarisha mtandao mkubwa zaidi unaowakilisha matabaka yote ya jamii za Iran.
Pia wamewaandama wanaharakati wa vyama vya wafanyakazi,wanafunzi na makundi ya kutetea haki za akina mama katika juhudi za kuhakikisha kwamba hawaungani na kuanza kugeuza mkondo wa kisiasa nchini.
Karroubi na Mousavi
Kama wenzao katika miji ya Cairo naTunis, wengi wa wafuasi wa upinzani waliojitokeza katika mitaa ya Tehran wiki hi ni kutoka kizazi cha Facebook .
Lakini wakati waandamanaji katika Misri waliungwa mkono na jeshi la nchi yao na pia serikali ya Marekani, mambo ni tofaut Iran .
Jeshi lenye nguvu la Walinzi wa Mapinduzi ndilo linaloongoza mapambano ya upinzani wowote dhidi ya serikali.
Na matamshi ya hadharani ya Rais Obama huenda kukaipa kila sababu serikali kuwashtumu wapinzani kuwa ni" wasaliti wanaoungana na Israeli " na kuwakandamiza.

Misimamo inayobadilika

Maandamano m,apya ya wiki hii yamewapa wafuasi wa vuguvugu la Green Movement supporters matumai mapya lakini wazi kua bado vuguvugu hilo liko mbali sana kuweza kuleta mageuzi ya kimsingi yaliyoshuhudiwa katika Misri au Tunisia.
Hata hivyo baadhi ya wachunguzi ndani na nje ya Iran wanasema wanaona upinzani umeanza kubadilika.
Shutuma za waandamanaji siku ya Jumaatatu zililengwa dhidi ya kiongozi mkuu wa utawala wa Iran - Ayatollah Khamenei.
Baadhi yao walitia moto picha zake na hata kudai auwawe-jambo ambalo usingeweza kufikiria kabla ya uchaguzi wa 2009 .
Kwa kuwatenga viongozi wa vuguvugu la KIJANI kutoka kwa mashina yao ya vijana, serikali huenda umeusukuma upinzani katika mkondo wa msimamo mkali zaidi. 
Mousavi na Karroubi wakiwa bado wanashikilia kuleta mageuzi ndani ya mfumo wa hivi sasa, hasira zinazozidi kupamba moto kama zilivyoshuhudiwa mitaani wiki hii zinaonyesha kuwa baadhi ya wafuasi wa upinzani huenda wasiridhike na mageuzi na sasa wanalenga kufanyike "mapinduzi.'

No comments: