ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 16, 2011

Majeruhi wa mauaji ya Selous apelekwa Muhimbili

Joseph Zablon 
MAJERUHI aliyenusurika katika tukio la mauaji ya watu wawili ambao waliopigwa risasi baada ya kupotea njia na kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Selous, Mfanyeje Kigwiso, amepelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.  

Ndugu wa majeruhi huyo Mohamed Suta aliliambia gazeti hili jana kuwa Kigwiso aliondolewa Kisarawe juzi na kupelekwa katika hospitali hiyo ya Taifa kutokana na hali yake kuendelea kuwa mbaya.  “Jeraha linalomsumbua zaidi ni lile la risasi aliyopigwa nyuma ya bega  na kutokea sehemu ya mkono kwa mbele,” alisema Suta na kuongeza:  "... Sasa analalamika kutokana na maumivu makali anayopata kutokana na jeraha hilo, hatujui hatima ya mkono wa kulia wa ndugu yetu ambao sasa haufanyi kazi."  


Katika hatua nyingine, kamisheni wanazopewa askari wa wanyamapori kutokana na kukamata au kuzuia ujangili ni ndogo na ndizo zinachangia mauaji ya raia wasio na hatia wanaoingia au kupita jirani na Hifadhi ya Selous, eneo la jirani na Mkoa wa Pwani, imeelezwa.  

Katibu Mkuu wa Chama cha Wawindaji  Mkoa wa Pwani, Johnson Nducha alisema kuwa kila askari wa wanyamapori anayeripoti kupambana na majangili hata kama hatawakamata, ili mradi tu risasi zimetumika, analipwa asilimia 30 ya mshahara wake.  "Inapotokea wakakamatwa watuhumiwa wa ujangili, kitu cha kwanza kinachofanyika ni kutaifisha mali zao yakiwemo magari, silaha na zana zingine za kuwindia na askari hao hulipwa kiwango hicho cha asilimia baada ya tathmini kufanyika kujua thamani halisi ya mali zilizokamatwa," alisema.  

Nducha alibainisha kuwa Septemba mwaka jana, askari mmoja alituzwa asilimia 30 ya Sh1.5 milioni kutokana na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa wa ujangili wakati kesi hiyo ikiwa bado inaendelea mahakamani.  

“Mimi nafikiri ni aina fulani ya ufisadi kwa sababu haiwezekani mtu alipwe bonansi hiyo ya kazi nzuri wakati shauri halijatolewa maamuzi mahakamani. Vipi kama mtuhumiwa akishinda kesi? Ina maana hizo pesa atarudisha au ndio inakuwa imeliwa Serikali?” alihoji Nducha.  Aliongeza"... kumbe mauaji ya namna hiyo yanaweza kuongozwa na tamaa ya kamisheni."  Katibu huyo alisema kuwa kuna wanachama wao ambao walikuwa na vibali vyote vya kuwindia katika hifadhi hiyo na walikamatwa.  

"Wafanyakazi hao walijeruhiwa na mali zao kushikiliwa. Jambo la ajabu zaidi wakati shauri lipo mahakamani, askari waliohusika katika operesheni hiyo, wakalipwa kamisheni zao," alisema. 


CHANZO:MWANANCHI 

1 comment:

Anonymous said...

Hi

Tunaona wananchi tunavyojiua sisi wenyewe jamani kwa hili ni bema Mkurugenzi na Mhihadhi wakawajibika! ni aibu! tena tumesikia baada ya kufanya mauajo hayo waliwatupa PORINI yaani miili yao na kisha ikaliwa na FISI na kubakia VICHWA TU na ndo vilivyo zikwa sasa Mh, Rais au waziri kweli mnaliacha jambo hili hewani tu! ipo siku wajomba zenu nao watafanyiwa hivyo kisha Serikali itachukua hatua but not foe this people???