ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 16, 2011

Mama, mtoto wafa kwa kula egg chops

Watu wawili, mama na mwanawe wamekufa baada ya kula ‘egg chops’ walizonunua kwenye duka la kuuzia mikate la Royal Oven Bakery lililopo Kawe, jijini Dar es Salaam.
Waliokufa ni mtoto Faidha Shabani (4) na mama yake Kharafa Shabani, wakati mume wake, Shabani Mgala, amelazwa hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam kwa matibabu, akiwa na msaidizi wa ndani ambaye jina lake halijafahamika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema wanamshikilia mmiliki wa duka hilo kwa mahojiano kuhusiana na vifo hivyo, ingawa hakumtaja jina lake.
Alisema wamechukua mabaki ya chakula kilichopatikana nyumbani kwa marehemu na kukipelekea kwenye mamlaka husika kwa uchunguzi.

Nyumbani kwa marehemu tumechukua mabaki ya egg chops pamoja na samaki ambazo walizinunua sehemu nyingine na kula, tumezipeleka mamlaka husika kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema Kamanda Kenyela.
Katika tukio hilo, watu wengine saba wamejitokeza na kuelezea jinsi walivyosumbuliwa na matatizo ya tumbo ambapo uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa walikula chakula chenye sumu.
Walisema walianza kusikia maumivu ya tumbo mara tu baada ya kula chakula hicho.
Hassan Juma, ambaye ni mkazi wa Mlalakua jijini Dar es Salaam, alisema mke wake, Joha Hassan (36), mtoto wake Naila Hassan (11) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi ya Al Muntazir na shemeji yake Aziz Almas (26) mwanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE) walipatwa na tatizo hilo.
Alisema tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita wakati wakitokea Bagamoyo kuwaangalia watoto wake wengine wanaosoma huko.
Alisema wakati wanarudi jijini Dar es Salaam walipita kwenye duka hilo na kununua egg chop nne, sambusa moja na maandazi kadhaa.
Alisema baada ya kuingia kwenye gari tayari kwa safari ya kuelekea nyumbani kwake Mlalakua, alichukua moja ya egg chop na kutoa sehemu ya juu ambayo ilikuwa na mafuta mengi na kumpatia shemeji yake kisha yeye akala yai lenyewe.
Nilishindwa kula sehemu ya juu ya egg chop kwa sababu ilikuwa na mafuta mengi ambayo mimi sipendelei, hivyo mke wangu, mtoto na shemeji yangu walizila zote,” alisema.
Alisema saa 7:00 usiku mke wake alianza kulalamika maumivu ya tumbo na kuanza kutapika na kuharisha na hali hiyo pia ilimtokea shemeji yake aitwaye Aziz Almas.
Alisema hadi jana asubuhi hali zao zilikuwa mbaya hivyo alilazimika kuwapelekea hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam kwa matibabu.
Alisema ilipotimia saa 9:00 alasiri, alirudi nyumbani na kumkuta mtoto wake, Naila ambaye alikuwa amerudi shule akiwa na hali mbaya.
Alisema alimpeleka hospitali na baada ya kuchukuliwa vipimo vyote vikiwemo X-Ray na Ultra Sound alibainika kuwa na sumu mwilini.
Alisema familia yake ililazwa hadi jana waliporuhusiwa kwenda nyumbani.
Kwa sasa wako nyumbani lakini hali ya kuharisha bado inaendelea, lakini nimesikitishwa na kauli ya mmiliki wa duka hili ambaye aliueleza umma kupitia televisheni kuwa tatizo la egg chop lilitokana na mayai na sio unga uliowekwa juu, hii sio kweli kwa sababu mimi nilikula yai na sijadhurika, tatizo ni ule unga wa juu ya yai,” alisema.
Naye Aziz ambaye alipatwa na janga hiyo, alisema kuwa saa kadhaa baada ya kula chakula hicho, alianza kusikia maumivu ya tumbo na alianza kuharisha na kutapika.
Kwa sasa nasikia kizunguzungu na maumivu ya kichwa, lakini bado naharisha,” alisema.
Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) tayari imefunga duka hilo ili kupisha uchunguzi wa kadhia hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: