
Luqman Maloto
Ukiangalia kwa makini, uhusiano wa watu wengi umekuwa ukiingia kwenye migogoro ya namna mbalimbali kwa sababu ya fedha.
Hili ni tatizo kubwa na ndiyo maana hii si mara ya kwanza kulizungumzia.
Bado nasisitiza kuwa inawezekana fedha si kila kitu, pia inaweza isiwe chochote. Hata hivyo ndiyo inayotusaidia kuishi pamoja na kufanya mambo mengine yenye kufurahisha na anasa mbalimbali.
Ukiangalia kwa makini, uhusiano wa watu wengi umekuwa ukiingia kwenye migogoro ya namna mbalimbali kwa sababu ya fedha.
Hili ni tatizo kubwa na ndiyo maana hii si mara ya kwanza kulizungumzia.
Bado nasisitiza kuwa inawezekana fedha si kila kitu, pia inaweza isiwe chochote. Hata hivyo ndiyo inayotusaidia kuishi pamoja na kufanya mambo mengine yenye kufurahisha na anasa mbalimbali.
Bila shaka unapojumuika na unayempenda huku mfuko ukiwa umenona, ni furaha iliyoje! Fedha hutupa nguvu na kujiamini katika kutekeleza njozi na matarajio. Sidhani kama kuna anayeweza kubisha.
Ukiachana na hulka ya kubisha kila kitu, tutakubaliana kwamba mafanikio yoyote nyuma yake huwa kuna kionjo cha fedha! Zinaheshimiwa kwa sababu zina nguvu! Hata hivyo, hazipaswi kukuongoza na kuamua sura ya maisha yako ya kimapenzi.
Hasara utakayoipata ni kuwa si ajabu mbele ya safari ukaonekana mwenye tamaa, kwamba unapenda kwenye noti au ukapondwa kwa ubahili wako hasa unapokuwa na mkono wa birika kipindi ambacho mwenzio anasumbuliwa na shida.
Wapendanao wengi waliachana baada ya mmoja kuingiwa na tamaa ya kutaka zaidi ya kile anachokipata kutoka kwa mwenzi wake. Hakuna ubishi kuwa binadamu wote wangekuwa na uwezo sawa kiuchumi, uaminifu ungekuwa wa kiwango cha juu.
Tafsiri ya neno “penzi la kweli” ingekuwa na maana inayojitosheleza. Nasema hivyo kwa sababu kama si wewe, basi shosti wako anamkaanga mwenzi wake kwa kutoa ‘halua’ kwa mtu mwingine.
Mada hii ina lengo la kukutaka ushinde majaribu hasa unapokuwa huna fedha au mwenzi wako anapotikiswa kiuchumi. Mantiki ni kwamba siku hizi hali ni mbaya na mapenzi ya kweli yamekuwa adimu kwenye ukata. Wengi wanazugwa!
Wengine wamekuwa na woga wa kujishughulisha na aina fulani ya watu, kwa kuona kwamba wenye fedha wakiamua, watawanyang’anya. Mfano ni huu: Kimati ni muuza genge eno la Yombo Machimbo, siku moja alinitamkia kuwa mwanamke mzuri hamtaki.
“Mimi mwanamke mzuri simtaki, uwezo wangu mdogo, nitanyang’anywa!” Ni kauli ya unyonge yenye kuumiza kutoka kwa Kimati. Anachokisema ni kweli lakini kuna mwanafasihi aliwahi kushauri kwamba “usiogope ukubwa wa samaki, uliza bei.”
Nakubaliana na ukweli kwamba kwenye migogoro ya fedha, pale ambapo salio halitoshi na madeni yanasumbua, kwa baadhi ya watu husababisha mtikisiko wa kimapenzi.
Maumivu mara mbili, mtikisiko wa uchumi na kupoteza mpenzi. Haya ni mabadiliko ambayo hayaepukiki na wapenzi wengi yalipowafika, walipena mkono wa kwa heri bila kupenda. Inauma kupita kiasi.
Hii ni kwa sababu unapotoka kwenye maisha ya utulivu, yaliyojaa starehe, kwenda kwenye mabadiliko ya kiuchumi ambayo kila mmoja huwa hapendi itokee, husababisha msongo wa mawazo kwa wahusika na kuchochea uvumilivu ukome haraka. Hivyo basi, penzi huingia mdudu kabla ya kuwa mwanzo wa kutengana.
Inapotokea kwamba kiwango cha uvumilivu kimekuwa finyu kwa wawili wanaopendana, husababisha maudhi ya hapa na pale, kero zisizo na maelezo ya kutosha kutokana na shaka ambayo hutawala fikra za kila mmoja kwenye uhusiano.
Je, unayo imani kwamba tatizo la fedha linaweza kuharibu muungano wako wa kimahaba na mwenzio? Inawezekana lakini siyo kihivyo! Kwa migogoro yote ya fedha uliyonayo leo, haitofautiani na ile ambayo itakufika siku za usoni. Maumivu ni ya wawili, ni vizuri kuvumiliana, kushikamana ili kuvuka vizingiti.
Kitu muhimu cha kufanya ni kushirikiana, kuepuka kugeukana na kucheza mchezo wa lawama. Huyu amuone mwenzake ndiyo chanzo cha tatizo. Zingatio ni kwamba mapenzi yakishamiri, kwa kiasi fulani hupunguza mawazo yanayosababishwa na ukata.
No comments:
Post a Comment