Advertisements

Wednesday, March 30, 2011

Dawa ya 'Babu' yasababisha mlundikano wa ARV's

BAADA ya Serikali kutangaza dawa ya Mchungaji Mstaafu Ambilikile Mwaisapile wa Loliondo, kuwa haina madhara kwa binadamu, huenda ikawa sababu ya vituo vingi vinavyotoa dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARVs) mkoani Manyara vikashindwa kutoka huduma hiyo. 

Hayo yalisemwa na Mratibu wa Afya, Uzazi wa Mama na Mtoto mkoani Manyara, Elizabeth Malley wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Mama na Mtoto yaliyotolewa na Shirika la Engender Health linalofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID), kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
 

Malley alisema katika mafunzo hayo yanayowashirikisha wakunga na wauguzi mbalimbali wa halmashauri sita za Mkoa wa Manyara, kuwa kutolewa kwa dawa ya Mchungaji Mwaisapile imekuwa changamoto kubwa kwa watumiaji wa ARV’s, ambao pia Serikali inatakiwa kuzidi kuwahamasisha kuendelea kuzitumia licha ya kujenga imani kwamba wamepona baada ya kutumia dawa ya Babu. 

Aidha, alisema tangu kuanza kuvuma kwa dawa hiyo ya Babu mwanzoni mwa Februari mwaka huu, imeelezwa kwamba misururu ya watumiaji wa vidonge vya ARV's katika vituo hivyo, imepungua, hali ambayo imesababisha kuwepo kwa mlundikano wa dawa hizo zinazokosa watumiaji katika vituo hivyo. 

Alisema ingawa idadi kubwa ya watumiaji wa ARV’s wamekwenda Loliondo kunywa dawa hiyo licha ya kuwepo kwa imani ya kupata uponyaji wa dawa hiyo, lakini mpaka sasa hakuna mtu mwenye Virusi vya Ukimwi anayetumia ARV’s aliyekuwa tayari kujitangaza. 

"Naomba wale wote waliokunywa dawa kwa Mchungaji Loliondo waje kwenye vituo wakiwa na vyeti vyao vinavyoonesha kuishi kwa VVU, halafu tuwapime kuthibitisha kama kweli wamepona baada ya kunywa kuliko kuacha kuendelea kutumia ARVs,” alisema Malley. 

Aidha, aliwasisitizia wateja wa Babu kuendelea kutumia vidonge vya ARV’s na kinga maalumu ya kujikinga na maambukizi wakati wa kujamiana kama hawajawa tayari kujitangaza na kuthibitika kuwa wamepona ili kuepusha ongezeko la maambukizi ya virusi hivyo. 

Akizungumzia hali ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, alibainisha kuwa bado kumekuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ongezeko la virusi hivyo mkoani Manyara kutokana na wanaume walio wengi kutokwenda na wake zao kliniki kupima afya zao.

No comments: