
Yanga na Simba leo zinakutana katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayofanyika leo kuanzia saa 10:00 jioni kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Timu hizo mbili zinashuka dimbani zikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi zao za ligi zilizopita ambapo Yanga inayoongoza iliifunga Ruvu Shooting 1-0 wakati mahasimu wao Simba walipata ushindi mnono wa magoli 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Manungu mkoani Morogoro.
Kocha wa Yanga, Sam Timbe, ambao ndio wenyeji wa mchezo huo, ameliambia gazeti hili kuwa maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika na ushindi ndio jambo analolitarajia.
Timbe alisema kuwa kwake mechi zote za ligi ni muhimu lakini atafurahi zaidi kuona anawafurahisha mashabiki wa Yanga ambao wanasubiri kuona timu yao inapata pointi tatu.
"Tuko tayari, muhimu ni kupata pointi tatu katika mchezo huo, hicho ndio tunachosubiri," alisema kwa kifupi Timbe ambaye amejiunga na Yanga akitokea Atraco ya Rwanda.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Davis Mosha, alisema kwa upande wa utawala kila kitu kimekwenda vizuri na wanachosubiri ni kuendeleza ushindi dhidi ya watani zao.
Mosha alisema kuwa hawataki kuchukua ubingwa peke yake ila malengo yao pia ni kuwafunga Simba mechi zote mbili kama wao walivyopoteza msimu uliopita.
Mzambia, Patrick Phiri aliliambia gazeti hili jana kuwa wachezaji wake wako tayari kwa mchezo huo na wameahidi kuendeleza kasi yao ya ushindi.
Phiri alisema kuwa hana hofu na majeruhi kwa sababu kila mchezaji aliyeko Simba ana uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya mbili na hivyo mapengo yatazibwa.
"Kila kitu kimekwenda kama tulivyopanga, tunasubiri muda ufike tuanze kazi tuliyoisubiri kwa zaidi ya wiki sasa," alisema Phiri.
Aliongeza kwamba licha ya mchezo huo kuwa na upinzani wachezaji wake wamejipanga ili kushinda na kuongeza ari ya kwenda kuwavaa mabingwa watetezi wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, TP Mazembe.
"Ni mechi ngumu lakini inatufanya wachezaji tujuwe jukumu letu na nini tunakihitaji baada ya kushinda, mpira ndio maisha yetu, kila mmoja amepanga kuonyesha anaweza kwa kufanya vizuri," alisema nahodha wa Simba, Nico Nyagawa.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema kuwa mashabiki wa timu hiyo wasiwe na wasiwasi wowote kwa sababu timu yao imeandaliwa katika kiwango cha juu.
Kaburu alisema kuwa maandalizi ya Simba yalianza tangu mzunguko huu wa pili ulipoanza na ana matumaini watachukua pointi tatu.
Katika mechi ya leo langoni mwa Simba anatarajiwa kusimama Ally Mustapha 'Bathez' huku Mbwana Samatta, Patrick Ochan, Amri Kiemba na Mussa Hassan ' Mgosi' wakiongoza mashambulizi wakati Yanga golini anatazamiwa kukaa Mghana, Yaw Berko na mbele Jerry Tegete, Davis Mwape na Iddi Mbaga, huku kuumia kwa Ernest Boakye huenda kukampa nafasi Athumani Iddi 'Chuji' katika nafasi ya kiungo.
Simba ilirejea jijini jana mchana ikitokea Zanzibar ilikokuwa inajifua tangu Jumatatu wakati Yanga watarejea mjini leo wakitoka Bagamoyo na kuelekea moja kwa moja uwanjani.
Kocha wa zamani wa Yanga, Mserbia, Kostadin Papic, aliyeiacha timu hiyo kutokana na kutofautiana na viongozi amewatabiria Simba ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo ushindi wa 2-0.
Yanga wanashuka dimbani wakiwa ndio vinara katika msimamo wa ligi huku wakiwa na pointi 38 wamecheza mechi 17 wakati Simba ni wa pili kutokana na kujikusanyia pointi 37 lakini wameshuka dimbani mara 16.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment