Dawa ya magonjwa sugu matano, inaelezwa yanapatikana kwa Babu Loliondo lakini tiba ya mapenzi kwa maana ya uhusiano, inatolewa hapa kwenye safu yetu ya XXLOVE. Karibu msomaji katika sehemu yetu hii ya tatu.
Nilipoanza kuchambua mada hii wiki iliyopita, nilieleza kuwa kila mtu anapenda, nikimaanisha kumpenda yule ambaye nafsi inakuwa imemdondokea. Lakini haijawahi kusemwa kwamba mapenzi ni utumwa.
Inawezekana ukawa hujapata mantiki ya hoja yangu hapo. Labda nikufafanulie kuwa tatizo linalowakabili watu wengi ni kushindwa kusoma alama za nyakati.
Namaanisha kutokufahamu kipimo cha mapenzi na wakati wake. Inawezekana alikupenda na unampenda lakini mabadiliko yake yakupe picha ili ujue cha kufanya.
Unangoja akuoneshe mpenzi mwingine ndiyo ujue kuwa zama zako zimefika tamati? Akufukuze kama mbwa na matusi juu? Usingoje aibu, heri nusu shari kuliko shari kamili.
Thamani yako ni kubwa mara sabini kama utakuwa mwelewa na kujiondoa kuliko taadhira ya kutupiwa virago. Kuna penzi hai na lililokufa, weka akilini na uheshimu.
Nilishafafanua mambo mengi kuhusiana na jinsi ya kulikabili penzi lililokufa, njia moja ambayo niliisisitiza ni kuinua mikono. Kulazimisha mapenzi ni gharama kubwa ambayo si rahisi kuifidia.
Hata hivyo, ni vema nikupe mbinu za awali. Hapa sitoi ushauri wa aina moja. Natoa njia nyingi ili uchague ya kushika kabla ya kupata suluhu.
Hapa chini kuna mambo ya msingi ya kufanya pale unapoona mwenzi wako amebadilika. Ukishindwa yote hayo, hapo hutakuwa na kufanya zaidi ya kuinua mikono. Uking’ang’ania, ni sawa na kukumbatia penzi lililokufa. Utateseka, utaaibika.
1.MSIKILIZE
Mpenzi wako anapokasirika na kukujia juu, unatakiwa umsikilize kwa makini. Mpe nafasi ya kuzungumza hata kama unahisi anakuonea. Kwa kufanya hivyo ataona umemheshimu na kumjali, hasira zake zitapungua. Katika utulivu na usikivu, suluhu ya kweli hupatikana.
2. JIDHIBITI
Mwenzi wako anapopanda juu kwa hasira na ghadhabu, hupaswi kuoneshana naye ubavu. Jifanye mjinga na dhibiti hisia zako, atatulia. Kujaribu kubishana kutafanya tatizo liwe kubwa zaidi. Hata kama anatoa maneno ya kukasirisha, jidhibiti kuepusha shari zaidi.
3. MKUBALIE ANACHOKITAKA
Unapoonesha kiburi au dharau kwa mpenzi wako anapokuwa amekasirika, tambua kwamba unaongeza ukubwa wa tatizo. Kama anakung’ang’aniza kukubali jambo ili aibuke mshindi, mkubalie ili mfikie muafaka. Hata kama unaona anachokulazimisha siyo sahihi, kubali kwa wakati huo, hasira zake zikitulia utazungumza naye vizuri.
4. CHUNGUZA KINACHOMKASIRISHA
Wapenzi wengi hulalamika kuwa wenzi wao hurudi majumbani wakiwa tayari na hasira. Hivyo kunapotokea jambo dogo ambalo huenda ni la kawaida, huhamisha hasira zao. Mchunguze mwenzi wako kugundua kinachomfanya akasirike.
Kama hukwazika anapokuwa kazini, akirudi jitahidi kumpa muda wa kutuliza akili na mfariji kwa maneno mazuri, hasira zake zitaisha. Kama hukasirika na uchafu wa mahali mnapoishi, jitahidi kuwa msafi na atazidi kukupenda.
5. USICHOCHEE MOTO
Unapoona mwenzio amekasirika, tambua kuwa moto wa hisia za kuumiza unamuwakia. Ni kosa kuendelea kumletea masihara katika wakati kama huu au kufanya makosa yatakayozidisha hasira zake. Jitahidi kumhudumia kama mtoto mdogo anapolia. Mbembeleze kwa maneno na vitendo, atarudi kwenye hali ya kawaida. Epuka kauli kama ‘jambo dogo tu linakuudhi?’ au ‘unakasirika hata bila sababu’.
6. USILALAMIKE
Hata kama unaona mwenzi wako anakutuhumu kwa jambo ambalo hujafanya au lisilo la kweli, hutakiwi kuanza kumlalamikia kuwa anakuonea. Tulia na mwache hasira zake zitulie. Baadaye utakapoona ametulia na kurudi kwenye hali yake ya kawaida, zungumza naye kwa upole na mweleze yale yaliyo moyoni mwako. Lawama huchochea zaidi hasira.
Itaendelea wiki ijayo.

No comments:
Post a Comment