ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 28, 2011

Chenge: Sijui kama mimi ni gamba CCM

MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge amesema anasubiri taratibu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuona kama atapewa barua ya kumtaka ajivue nafasi zake za uongozi kwani hadi hivi sasa hajui kitu hicho.Kauli hiyo ya kwanza ya Chenge inakuja kipindi ambacho Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amekuwa akitangaza kwa nguvu mpango mkakati wa chama hicho kujivua gamba.

Makada wa chama hicho wanaotakiwa kupima nafasi zao na uzito wa tuhuma zinazowakabili ni wale wanaohusishwa na kashfa mbalimbali zikiwamo za Richmond, Kagoda na wizi wa EPA.

Hata hivyo, Chenge jana alipoulizwa na gazeti hili kuhusu kutajwa kwake kuwa mmoja wa wanachama wanaotakiwa kupima uzito wa tuhuma zinazowakabili na kujiondoa wenyewe ikiwa ni hatua ya chama hicho kujisafisha kwa kujivua gamba, alisema: "Sijui hicho kitu. Naheshimu vikao na taratibu za chama hilo ni jambo la chama si la vyombo vya habari."

Alisema chama kina taratibu zake za kiutendaji na kuongeza: "Siwezi kuanza kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu mambo ambayo yana taratibu zake ndani ya chama."

Alisema kamwe hatakiuka taratibu za chama na kwamba uamuzi wote utakaofanyika au kutolewa huwa unafuata vikao vya chama.Alipoulizwa juu ya kusubiri kwake taratibu za chama wakati tayari jambo hilo linafahamika kwa umma alijibu: "Kwa ‘public’ ipi wewe? Mimi sijui hilo jambo, nasubiri taratibu za chama na siwezi kuzungumza zaidi nje ya chama."

Akizungumzia utekelezaji wa maazimio ya Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC-CCM), Nnauye alisema taratibu zimekuwa zikiendelea na kuwataka wananchi kuwa na subira.Juzi, Nnauye alikaririwa akisema kwamba taratibu hizo zingefanyika baada ya Sikukuu ya Pasaka na kusisitiza: "Ambacho nimekuwa nikikisema kiko palepale."

Mapema mwezi huu, NEC-CCM ilitoa muda wa siku 90 kwa watuhumiwa wote wa kashfa mbalimbali ndani ya chama hicho kujipima wenyewe na kujiondoa kwenye nafasi hizo vinginevyo, chama kingewang'oa kwa nguvu. Azimio hilo limekuwa likitangazwa kwa nguvu katika mikutano mbalimbali ya hadhara ikiwa ni mkakati wa chama hicho kurejesha imani  chama kwa wananchi ambayo imeanza kupotea kutokana na tuhuma za ufisadi.

Juzi, Nnauye akizungumza na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC Taifa), alisema chama hicho hakitishiki na uwezekano wa makada hao kuhamia upinzani.

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akihutubia sherehe za kuzaliwa chama hicho Februari 5, mwaka huu alitangaza mkakati huo wa chama kujivua gamba na kurejea katika misingi ya maadili ya uongozi iliyorithi kutoka Tanu na CCM ya nyuma.

Sekretarieti ya CCM kukutana kesho
Katika hatua nyingine Sekretarieti ya CCM inatarajiwa kukutana kesho kujadili pamoja na mambo mengine, utekelezaji wa maazimio ya Nec-CCM.

Kwa mujibu wa duru za kisiasa kutoka CCM, mkutano huo utajadili ajenda hiyo kwa kufanya tathmini ya azimio hilo na namna ya utekelezaji wake.Alipoulizwa jana, Nnauye alithibitisha kufanyika kwa mkutano huo lakini alisema ni kikao cha utendaji cha kawaida.Kwa mujibu wa Nnauye, kikao kama hicho kiliwahi kufanyika Mjini Dodoma baada ya kuundwa kwa sekretarieti hiyo na pia tayari ilikwishakutana Dar es Salaam.

Alisema kikao hicho si maalumu wala cha dharura na kwamba hufanyika mara moja kwa wiki.
"Siyo kikao cha dharura wala kikao maalumu, ni sehemu tu ya utendaji wa sekretarieti. Tunafanya vikao kama hivi mara moja kwa wiki, kwa hiyo hakuna kikao maalumu," alisema.

CHANZO:MWANANCHI

No comments: