Diwani wa Kata ya Machochwe mkoani Manyara kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Samwel Chacha Gibewa, anadaiwa kukutwa ameficha bunduki ya kivita aina ya AK 47 shambani kwake.
Polisi wamesema silaha hiyo imekuwa ikitumika katika matukio mbalimbali ya uhalifu.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Enos Mfuru, ndiye alimlazimisha diwani huyo kufukua bunduki hiyo iliyokuwa imefichwa katika shamba lake.
Mkuu huyo wa Mkoa alifikia hatua hiyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba, diwani huyo anamiliki silaha kinyume cha sheria na imekuwa ikitumika katika matukio ya uhalifu, yakiwemo ya ujambazi, wizi wa mifugo na uwindaji haramu wa wanyama katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Edward Ole Lenga, baada ya mkuu wa mkoa kupata taarifa hizo, alimfuata diwani huyo na kumtaka aisalimishe silaha hiyo, kama walivyofanya wananchi wengine wilayani humo.
Hata hivyo, alisema diwani huyo alikataa kwamba hana silaha lakini mkuu wa mkoa alipomweleza kwamba hatamchukulia hatua zozote za kisheria, alikubali na kuwapeleka katika shamba lake la mahindi na walipoifukua waliikuta ikiwa na risasi 21.
‘Sisi tulipata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba diwani huyo anamiliki silaha kinyume cha sheria, tulimwambia aikabidhi lakini akasema hana, sasa juzi mkuu wa mkoa alipokuja hapa alimuomba kwanza alikataa katakata, baadaye alikubali na kutupeleka kwenye shamba lake na kuanza kuifukua na mkuu wa mkoa alimsaidia kuifukua,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kupatikana kwa silaha hiyo kumetokana na operesheni kabambe ya kusaka watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, tangu zoezi hilo lilipoanza Januari, mwaka huu, jumla ya bunduki 14 zikiwemo za kivita, zimekwishasalimishwa na watu mbalimbali wilayani humo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kituo cha Haki za Binadamu wilayani Serengeti, Samwel Mewama, alisema ofisi yake imesikitishwa mno na kitendo hicho na inawezekana ilishatumika katika matukio mbalimbali ya uhalifu.
Mwandishi wa habari hizi alipompigia simu diwani huyo ili azungumzie suala hilo hilo, simu yake ya mkononi haikupatikana.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment