.jpg)
Uongozi wa mabingwa wapya wa soka Tanzania Bara, Yanga ya jijini Dar es Salaam, jana ulimwongezea mkataba wa mwaka mmoja na kocha wake, Mganda, Sam Timbe, kwa ajili ya kuifundisha timu yao katika msimu ujao wa ligi na mashindano ya kimataifa.
Timbe, mara baada ya kufikia makubaliano na Yanga, aliondoka nchini na kurejea kwao Uganda kwa ajili ya mapumziko.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jana mchana kutoka kwa uongozi wa mabingwa hao, Timbe atarejea nchini Juni 15 ili kukiandaa kikosi chake na msimu huo.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa hata hivyo, Yanga, wataendelea kufanya mawasiliano na kocha wao katika zoezi zima la usajili itakapohitajika ushauri wake ili wawe na kikosi imara msimu ujao.
"Tunataka kufanya kazi kisayansi, hata akiwa mapumziko atakapohitajika kutupa ushauri tutakuwa tunawasiliana nane ili tuijenge Yanga iliyo imara na yenye ushindani zaidi," alisema kiongozi huyo.
Timbe alijiunga na Simba mapema mwezi Februari baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mserbia, Kostadin Papic, kuamua kuondoka nchini baada ya kutofautiana na viongozi wa timu hiyo.
Awali Timbe alisaini mkataba wa miezi mitatu na viongozi wameamua kumuongezea mkataba mrefu baada ya kuridhishwa na utendaji wake.
Mganda huyo ana rekodi nzuri katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambapo ameshawahi kuzipa ubingwa wa Kombe la Kagame klabu za Polisi Uganda, SC Villa na Atraco ya Rwanda mwaka 2009 wakiwa Khartoum nchini Sudan kwa kuwafunga wenyeji, El Mereikh.
Pia uongozi wa klabu hiyo umeshamsainisha kiungo wake, Nurdin Bakari, ambaye alikuwa akiwindwa na klabu yake za zamani ya Simba na Azam.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment