ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 16, 2011

Hatma ya Phiri, Kaseja Simba leo

Hatma ya kocha Mzambia Patrick Phiri na wachezaji ambao wamekuwa wakitajwa kuwa katika "mstari mwekundu" wa kutemwa na klabu ya Simba, inatarajiwa kujulikana leo wakati kamati ya utendaji ya klabu hiyo itakapokutana jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya kufanya tathmini ya msimu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliomalizika huku agenda kuu ikiwa ni kujua kikosi kipya cha timu hiyo kitakachopeperusha bendera ya Wekundu wa Msimbazi msimu ujao.

Akizungumza jana, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', alisema kuwa kikao hicho kinafanyika kufuatia kukabidhiwa kwa ripoti ya ufundi kutoka kwa ya kocha wao, Patrick Phiri.
Kaburu alisema kuwa katika kikao hicho watajadili ni jinsi gani timu yao iliyokuwa inaongoza katika msimamo wa ligi kwa muda mrefu kushindwa kutetea ubingwa wao na hatimaye watani zao kuibuka mabingwa wapya.
Alisema kuwa katika kikao hicho watajadili mikakati yao mipya kwa ajili ya msimu mpya ambao utatanguliwa na ushiriki wao kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame.
"Tumeshapokea ripoti ya Phiri, kwa hiyo tutajiuliza ni kwa vipi tulipoteza ubingwa tuliokuwa tunaushukilia na baada ya hapo kujipanga upya kuboresha kikosi chetu," alisema kiongozi huyo.
Kaburu alisema kuwa kila kitu kilichotendeka msimu wote uliomalizika kitajulikana katika kikao hicho ambacho pia kitapokea ripoti ya kamati yao ya ufundi.
"Hapo ndio tutakapojua kila kilichofanyika baada ya kupitia kwa undani ripoti ya kocha, kila kitu kitajulikana hapo," alisisitiza.
Alisema kuwa usajili wa kikosi chao kipya utafanyika kwa kuzingatia mapendekezo ya kamati ya ufundi na wanaamini utekelezaji wake ndio utakaoifanya Simba ya msimu ujao kuzaliwa mpya na kuwa yenye ushindani zaidi.
Aliongeza kuwa kutokana na kukabiliwa na mashindano ya Kombe la Kagame yatakayoanza kutimua vumbi kuanzia Juni 21, wanawalazimika kujipanga imara na kuhakikisha kila jambo linafanyika kwa umakini na kwa wakati.
Alisema mbali na ripoti ya kocha wao, pia viongozi wamepokea na wanaendelea kupokea maoni mbalimbali ya wanachama wao na watayafanyia kazi ili kufikia malengo ya kuwa na kikosi imara.
Wakati huo huo, Kaburu, alisema kuwa endapo mabingwa watetezi wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, TP Mazembe, watawasiliana nao ili kufanya taratibu za kumsajili mshambuliaji wao, Mbwana Samatta, hawatamzuia kama walivyowaruhusu nyota wengine akiwemo, Henry Joseph, Haruna Moshi 'Boban' na Danny Mrwanda.
Majina ya wachezaji nyota kadhaa akiwemo kipa Juma Kaseja, kiungo Mohammed Banka na washambuliaji Mussa Hassan na Mganda Emmanuel Okwi yamekuwa yakitajwa sana katika vyombo vya habari kama miongoni mwa waliokalia "kuti kavu" pamoja na kocha wao, Phiri.
Habari zilizotufikia jana, mabeki watatu wa Simba, Amir Maftah, Amri Kiemba na Haruna Shamte wamesaini mikataba mipya ya kuendelea kuichezea timu hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: