.jpg)
Spika wa zamani wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), almaarufu kama Bajaj, ni miongoni mwa wabunge walioibuka washindi katika kinyanganyiro cha kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.
Katika uchaguzi huo Lusinde ambaye alijipatia umaarufu mkubwa wakati alipomng’oa katika kiti cha Ubunge, Mzee Samuel Malecela katika Jimbo la Mtera, aliongoza kwa kujizolea kura 126 katika uchaguzi uliofanyika kujaza 10 za wajumbe wa NEC kupitia wabunge wa CCM.
Uchaguzi huo ambao ulimalizika juzi saa 6.00 usiku, ulifanyika katika ukumbi wa wa ukumbi wa Pius Msekwa Bungeni.
Wengine walioibuka washindi katika uchaguzi huo ambao unawapa nafasi ya kushiriki katika vikao vya juu vya chama hicho tawala na kura zao katika mabano ni, Mbunge wa Temeke, Abdul Mtemvu (110) na Spika wa zamani wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta (104).
Sitta ambaye hivi sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alikuwa mjumbe wa NEC na Kamati Kuu ya chama hicho kwa nafasi ya Uspika.
Hata hivyo, alipoteza nafasi hizo mara baada ya kupoteza kiti cha uspika.
Wengine waliibuka kidedea ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (88) na Mbunge wa Kigoma Mjini Peter Selukamba (70).
Wengine kwa upande wa wanawake Bara ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi), Hawa Ghasia,(98) Angela Kairuki (112) na Munde Andallah (72), ambapo kwa upande wa Zanzibar, walioshinda ni Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia ni Mbunge wa Muyuni, Mahadhi Juma Maalim na Mbunge wa Viti Maalum, Faida Bakari.
Wagombea wengine waliowania nafasi hizo lakini wakabwagwa katika uchaguzi hu ni pamoja na Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage, Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa AnnaTibaijuka.
Wengine ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mbunge wa Igalula, Athuman Mfuta Kamba na Matha Mlata wakati Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe alijitoa. Wajumbe hao watashikilia nafasi hizo kwa miaka 10.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment