Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imeamuru vyombo vya habari kuacha kuripoti ushahidi wa kesi ya madai ya Sh. Moja na kuitwa fisadi papa, iliyofunguliwa na mfanyabiasha Yusuf Manji dhidi ya Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, kwa sababu taarifa zinazotolewa na vyombo hivyo zinakinzana na kumbukumbu za kesi hiyo zilizopo mahakamani.
Kadhalika, mahakama hiyo imesema kukinzana kwa taarifa hizo kunaingilia uhuru wa mahakama pamoja na hakimu anayesikiliza kesi hiyo.
Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Illivin Mgeta, ambapo kesi hiyo ilipangwa kutajwa jana mahakamani hapo baada ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana, kujitoa kuisikiliza wiki iliyopita.
"Mahakama ni sehemu ya wazi ambapo kila mtu anaruhusiwa kuingia kusikiliza kesi, lakini kuanzia sasa vyombo vya habari marufuku kuandika ushahidi wa kesi hii kwa sababu taarifa zinazowafikia wananchi na kumbukumbu za kesi hiyo zilizopo mahakamani vinakinzana kwa hiyo kunavuruga mwenendo mzima wa kesi... ila vyombo vya habari vinaruhusiwa kuandika tarehe za kutaja tu," alisema Hakimu Mgeta.
Aidha, alisema hakimu atakayeendelea kusikiliza kesi hiyo atajulikana Juni 3, mwaka huu ambapo imepangwa kutajwa.
Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Katemana lakini alijitoa wiki iliyopita na kurejesha jalada kwa Hakimu Mfawidhi.
Awali, mawakili wa mfanyabiashara huyo waliomba mahakama kuondoa baadhi ya vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo kama ushahidi na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, kikiwemo cha kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd kuhusishwa na mteja wao.
Mengi aliwasilisha vielelezo 14 vya ushahidi kikiwemo cha Manji kuhusishwa na kampuni ya Kagoda ambayo ilitajwa kuwa ilihusika katika uchotaji wa mabilioni ya fedha kutoka Benki Kuu Tanzania(BoT).
Hata hivyo, mahakama ilikubali kuviondoa vielelezo hivyo.
Katika ushahidi wake, Manji alidai Aprili 23-27 mwaka 2009, Mengi kwa kutumia kituo cha Televisheni cha ITV, alitoa madai kuwa Manji na wafanyabiashara wengine kuwa ni mafisadi papa, wanahamisha raslimali za taifa kupeleka nje ya nchi na kwamba wameshiriki kikamilifu katika ufisadi wa ununuzi wa magari ya JWTZ, rada, mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma, mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSPF na NSSF, Dowans na Richmond.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment