ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 15, 2011

Kesi ya wizi wa fedha za EPA yaendelea kunguruma

Shahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi ya wizi wa Sh. bilioni 2.2, kwenye benki ya NBC, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kuwa, benki hiyo iliona fedha za kigeni zilizokuwa kwenye matawi yake ni mzigo kuendelea kukaa nazo na kuamua kuzirejesha Benki Kuu Tanzania na kufunguliwa Akaunti ya Madeni ya Fedha za Nje (EPA).

Maelezo hayo yalitolewa na shahidi wa upande wa Jamhuri, Lyson Mwakapenda (67), mbele ya jopo la mahakimu watatu, wakiongozwa na Jaji Beatrice Mutungi ambaye anaisikiliza kesi hiyo kwa kibali cha Jaji Mkuu wa Tanzania. Wengine wanaosikiliza kesi hiyo ni Mahakimu Eddie Fussi na Amir Msumi.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni, wafanyabiashara Japhet Lema mkazi wa jijini Arusha na Jonathan Munisi wa jijini Dar es Salaam, ambayo wanadaiwa kuhusika na wizi huo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Arafa Msafiri, akisaidiwa na Shadrack Kimaro, Mwakapenda ambaye ni Meneja Uhusiano wa Benki ya NBC Kimataifa, alidai kuwa alisimamia malimbikizo ya fedha za EPA zilizolipwa na wafanyabiashara nchini walioagiza bidhaa nje ya nchi.
Alidai kuwa baada ya uhaba wa fedha za kigeni nchini benki ya NBC ililazimika kufungua akaunti maalum ya fedha hizo, na kwamba benki hiyo ilifanya kazi hiyo kwa niaba ya BoT.
"BoT, hazina na NBC walikubaliana fedha hizo zihamishiwe benki kuu kutokana na NBC ambayo ilikuwa wakala kuona fedha hizo zimekuwa mzigo" alidai Mwakapenda.
Msafiri alidai kuwa wanatarajia kuwa na shahidi mwingine mmoja wa mwisho, ambaye kwa sasa wanaendelea kufanya naye mawasiliano kwa sababu yuko nje ya nchi.
Jaji Mutungi alisema upande wa mashtaka ufanye jitihada kuwasiliana na shahidi huyo ili kesi iendelee kusikilizwa na haki iweze kutendeka kwa pande zote mbili.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 19, mwaka huu na itaendelea kwa kusikilizwa ushahidi wa upande wa Jamhuri Juni 29 na 30, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: