.jpg)
Licha ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu, klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam haitashiriki michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) itakayofanyika Juni nchini Sudan na washindi kuzoa kitita cha dola za Marekani 100,000, sawa na Sh. milioni 150.
Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye alisema kuwa Yanga haitashiriki michuano hiyo kwavile bado haijamaliza adhabu yake ya kutumikia kifungo cha miaka mitatu.
CECAFA iliifungia Yanga katika mashindano yake na kuitoza faini ya dola 35,000 za Marekani mwaka 2008 baada ya kugoma kuingia uwanjani kucheza mechi ya kuwania mshindi wa tatu wa Kombe la Kagame dhidi ya mahasimu wao Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Musonye alisema kuwa Yanga bado haijamaliza adhabu yake ya miaka mitatu na vilevile, haijalipa faini waliyotozwa na kamati ya utendaji ya CECAFA.
Musonye alisema kuwa Yanga itaendelea kukaa nje ya mashindano hayo hata pale miaka mitatu waliyofungiwa itakapomalizika endapo hawatalipa faini.
"Tunawapongeza Yanga kwa kuwa mabingwa wa Tanzania Bara. Lakini kwa upande wa mashindano yetu, timu iliyoshika nafasi ya pili (Simba) ndiyo itashiriki mashindano ya Kagame," alisema Musonye.
Akifafanua kuhusu namna ya kuhesabu muda wa kifungo cha Yanga, Musonye alisema wanaangalia pale tu wanapokuwa wametwaa ubingwa wa nchi na kwamba hawahesabu mwaka ambao klabu hiyo haijafanikiwa kutwaa taji hilo.
Aliongeza kuwa CECAFA wameamua kutowafungulia Yanga ili iwe fundisho kwa timu nyingine kwani zote zinatakiwa kuheshimu mashindano hayo yaliyoanza kufanyika miaka zaidi ya 30 iliyopita.
Kutokana na adhabu ya Yanga, Simba walioiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya Kagame mwaka jana watashiriki tena michuano ijayo kwa sababu imemaliza ikiwa ya pili, nyuma ya Yanga.
Michuano ya Kagame ya mwaka huu itaanza kutimua vumbi kuanzia Juni 21 hadi Julai 5 jijini Khartoum, Sudan.
Awali, mashindano ya mwaka huu yalitarajiwa kufanyika Zanzibar lakini kukosekana kwa wadhamini wa kugharimia tiketi za ndege kwa timu zote zinazoshiriki, viongozi wa CECAFA, waamuzi pamoja na malazi na chakula kuliipa Sudan nafasi ya uenyeji.
Kampuni ya El Mereikh inayomiliki timu ya El Mereikh ndio imethibitisha kudhamini mashindano hayo mwaka huu, ikiwemo kuongeza fedha za zawadi na kufikia dola 100,000.
Tangu mwaka 2004, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, alikuwa akitoa dola 60,000 za Marekani (sawa na Sh milioni 90) na kutokana na ongezeko hilo, mwaka huu zawadi kwa bingwa, mshindi wa pili na wa tatu zitaongzeka.
APR ya Rwanda ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo ambapo mabingwa watetezi wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika, TP Mazembe, wakiwa waalikwa waligomea mechi yao ya Kundi C baada ya nahodha wao Tresor Mputu kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment