ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 15, 2011

Mapato Samunge vurugu tupu

Mchungaji Ambilikile Mwasapila
Mussa Juma, Samunge
UONGOZI wa Kijiji cha Samunge, umetoa siku mbili kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kuwaondoa maofisa wake wanaokusanya ushuru wa magari na helikopta zinazopeleka wagonjwa kijijini hapo kupata tiba inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwasapila, vinginevyo utasitisha utoaji wa tiba hiyo.
Uamuzi huo ulifikiwa jana katika Mkutano Mkuu wa Kijiji cha Samunge, uliofanyika kwenye Uwanja wa Nanenane na kuhudhuriwa na maofisa kadhaa wa Serikali, akiwamo mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ngorongoro, Bakari Gaima.

Akitangaza uamuzi huo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Michael Lengume alisema mkutano huo unamtaka mkurugenzi kuwaondoa maofisa wanaokusanya ushuru wa magari na helikopta ifikapo leo na kwamba kazi hiyo sasa itaanza kufanywa na wakusanya ushuru wa kijiji kuanzia Jumamosi.

"Kama halmashauri itakaidi agizo hilo, tutasitisha utoaji wa huduma ya tiba katika kijiji hiki baada ya kukutana na Mchungaji Mwasapila na kuyazuia magari," alisema.
Wakizungumza kabla ya kufikiwa uamuzi huo, Diwani wa Kata ya Samunge, Jackson Sandea, Kiongozi Mkuu wa mila wa Kabila la Wasonjo (Mwanamiji), Peter Dudui, Solomon Baragiswa, Mary Meano na Njuda Lemindi walisema mapato ya magari na helikopta ni haki ya kijiji hicho na siyo halmashauri wala Serikali Kuu pekee.

Sandea alisema kamwe hawatakikubali kitendo cha halmashauri kupora mapato hayo kwani Serikali ya Kijiji inatambuliwa kisheria na ina haki ya kukusanya mapato kama vilivyo vijiji vingine nchini.
"Huu ni uporaji wa mapato yetu, tulianza kukusanya vizuri na kutumia fedha katika kazi za usafi wa mazingira, kuchimba vyoo na kutumia katika miradi mingine lakini sasa wametuvamia na kuanza kukusanya wao," alisema diwani huyo na kuongeza:
"Katika vituo wanatoza fedha za vibali, wanachukua fedha za ukaguzi wa magari na nyingine nyingi tu ambazo zinalalamikiwa na wananchi. Kwa nini tena tuambiwe na huku kwetu fedha zinakusanywa kwa ajili yao?"

Dudui alisema viongozi wa mila wanapinga utaratibu wa halmashauri wa kukusanya mapato yote bila kueleza kijiji kitanufaika vipi na ujio wa maelfu ya watu."Sasa vyanzo vya maji vimechafuliwa, mashamba yameharibiwa kutokana na kutupwa taka mbalimbali kama chupa za maji, magari yameegeshwa mashambani, njaa itakuja. Je, nani atawasaidia hawa wananchi?" alihoji Dudui.
Kiongozi huyo wa kimila pia alieleza kushangazwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kuamua kupeleka Samunge watu wa kufanya usafi kutoka nje ya kijiji hicho akisema hatua hiyo inawanyima ajira vijana wa Samunge.

Kwa upande wake, Baragiswa aliwasihi wananchi wa Samunge kupunguza jazba kutokana na kuporwa mapato yao, akashauri taratibu za kiserikali zifuatwe ili haki ya kijiji kupata mapato irejeshwe.
 "Mimi sipendi kuwafukuza kwa nguvu watu wa halmashauri, dunia nzima sasa inatazama Samunge tusijichafue. Taratibu zifuatwe ili kijiji kikusanye mapato yake," alisema Baragiswa.Lemindi alisema Serikali za vijiji zinatambuliwa kisheria na halmashauri haiwezi kuingilia masuala ya kijiji bila majadiliano hivyo, ni busara suala hilo kumalizwa kisheria.

Katika mchango wake, Mary Meano alisema alilalamikia uwapo wa kina mama lishe wengi kutoka nje ya wilaya hiyo ambao walifika Samunge kupata tiba na sasa wamefungua migahawa ambayo haina huduma muhimu kama vyoo."Kina mama wa Samunge tunashindwa kufanya biashara. Kuna wageni wengi hapa bila utaratibu, tunaomba kijiji kiratibu ujio wao na kuweka utaratibu mzuri wa huduma za afya na vyoo hapa kijijini," alisema Meano.

Tangu Mchungaji Ambilikile Mwasapila aanze kutoa tiba ya magonjwa mwanzoni mwa mwaka huu, wastani wa magari 1,000 yanafika Samunge kwa siku, huku helikopta ikifanya safari kati ya nne na sita kwa siku.

Halmashauri Ngorongoro  yajivua lawama
Gaima aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, alisema haijapora mapato ya kijiji, bali inatekeleza uamuzi wa kikao cha wakuu wa mikoa inayopakana na Ngorongoro na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Gaima alisema kikao hicho kiliamua kuwa halmashauri ikusanye Sh5,000 kwa kila gari na kati ya hizo Sh3,000 zitapelekwa kusaidia vituo vya kuratibu magari yanayokwenda Samunge vya Bunda, Arusha, Longido na Babati na nyingine Sh2,000 zibaki halmashauri.

"Iliamuliwa mapato kukusanywa na halmashauri ili iwe rahisi kupatikana hizo 3,000 na kuhusu kijiji kuna utaratibu utaandaliwa ili kinufaike na pia ilionekana ni busara halmashauri kusimamia mapato ili kuratibu zoezi zima la usafi na utunzwaji wa mazingira," alisema Gaima.Kaimu Mkurugenzi huyo pia alikanusha uvumi kuwa uamuzi wa kutaka halmashauri ikusanye fedha, ulitokana na mapendekezo ya Mchungaji Mwasapila.

"Mchungaji alishirikishwa tu baada ya uamuzi kufikiwa hasa baada ya idadi kubwa ya watu kufurika hapa ambapo ilisababisha watu kufariki kutokana na kukosa huduma," alisema Gaima.
Akizungumzia ajira kwa vijana wa Samunge, Gaima alisema waliamua kutafuta vijana kufanya kazi za usafi kutoka nje ya Samunge baada ya kupata taarifa za vijana wa Samunge kugoma kufanya usafi.

Wahandisi wa JKT watua Samunge
Hatimaye wahandisi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), juzi walitua Samunge kuainisha maeneo ya kuchimbwa vyoo ili kuimarisha usafi lakini kabla ya kufanya lolote walipata kikombe cha tiba.

 Wahandisi hao walikuwa wameandamana na Diwani wa Samunge, Sandea na ujio wao ilielezwa kuwa ni wa kuchimba vyoo na kuboresha mazingira ya usafi. Bado huduma za vyoo na usafi ni mbaya katika Kijiji cha Samunge na vijiji vya jirani na pia uchafu umezagaa barabarani kuanzia Kigongoni hadi Samunge na Loliondo.

CHANZO:MWANANCHI

No comments: