Wataka ishughulikiwe kwa uadilifu, umakini mkubwa
Pia waasa vyama vya siasa kutopenyeza ajenda za siri
Pia waasa vyama vya siasa kutopenyeza ajenda za siri.jpg)
Maaskofu nchini wametahadharisha kwamba bila kuwepo umakini katika mchakato wa kupata Katiba Mpya, nchi inaweza kuingia katika matatizo.
Maaskofu hao walitoa angalizo hilo katika mahubiri yao ya sikukuu ya Pasaka ya kuadhimisha kumbukumbu kufufuka kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2,000 iliyopita.
Askofu Msaidizi Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, alisema mchakato wa kupata Katiba mpya lishughulikiwe kwa uadilifu, umakini na umahiri mkubwa kwa sababu katiba sio ilani ya chama cha siasa.
Askofu Nzigilwa alivitahadharisha vyama vya siasa kutopenyeza ajenda za siri kwenye suala kuu la kitaifa kama katiba.
Alisema nchi sasa ipo katika mchakato wa kuandika Katiba mpya na kwa bahati mbaya dalili za ushabiki wa kisiasa zimeanza kujitokeza, jambo alilosema ni hatari kwa taifa.
“Nashukuru rasimu ya katiba imerudishwa kuandikwa upya, wito wangu kwenu mshiriki kikamilifu kwenye mchakato wa kupata katiba mpya na ni vyema tuepukane na itikadi ya vyama vya ki siasa,” alisema Askofu Nzigilwa wakati wa mahubiri yake katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, jijini Dar es Salaam.
Alisema Katiba mpya haitakuwa na maana endapo kusudio kubwa ni kukiondoa chama kinachotawala madarakani bali kunufaisha vizazi viliopo na vijavyo.
Aidha, aliwaasa Watanzania kuwa na utamaduni wa maridhiano kwa kuwa wakweli kuanzia ngazi ya familia kama njia ya kuuenzi ufufuo wa Yesu.
Askofu wa Kanisa Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Askofu Thomas Laizer, amewataka waumini wa madhehebu ya Kikristo kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho taifa linaelekea kwenye mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya ya nchi.
Aidha, Askofu Laizer aliwataka Wakristo waepuke kutumiwa na watu wenye nia mbaya ya kuliingiza taifa katika machafuko.
Katika mahubiri yake kwenye ibada ya Pasaka katika Usharika wa Mjini Kati, Askofu Laizer alisema Wakristo wanapaswa kuomba hekima kutoka kwa Mungu ili waweze kutoa maoni yatakayosaidia kupatikana kwa katiba itakayosimamia haki, wajibu na kuendeleza umoja wa kitaifa.
Askofu Laizer aliongeza kuwa Serikali inapaswa kuhakikisha hisia za tofauti za kidini, kikabila na udini hazipenyezwi katika mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya.
Alisema katika siku za karibuni, vimeibuka vikundi vya kidini ambavyo vinaendesha mihadhara ya kashfa dhidi ya dini nyingine, hali ambayo isipodhibitiwa inaweza kuleta vurugu na maafa nchini.
Askofu Shao wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, alisema suala la mabadiliko ya Katiba mpya serikali ilichukue kwa uzito wa pekee kuhakikisha wananchi wanapewa nafasi ya kutosha kuamua aina ya katiba wanayoitaka.
“Tunawaasa viongozi wetu wazingatie hisia na wawe waangalifu kutotumia madaraka kuonyesha kwamba wapo wenye haki zaidi kuliko wengine. Katiba inayotarajiwa ni ya Watanzania wote,” alisema wakati wa mkesha wa ibada ya Pasaka juzi katika Kanisa la Minara Miwili mjini Zanzibar. Kwa upande wake, Kasisi Kiongozi wa Kanisa Anglikana Zanzibar, Emmanuel Michael, aliwataka wananchi wa Zanzibar kujitokeza kutoa maoni ya Katiba wakati mwafaka ukifika na kujiepusha na jazba ili lengo la kuwa na Katiba mpya liweze kufanikiwa.
Naye Mchungaji Idan Kamote wa Mtaa wa Mtakatifu Barnaba wa Kanisa la Anglikana Kange, jijini Tanga, alisema mjadala wa Katiba mpya ni changamoto kubwa kwa Taifa kwa kuwa unayahusisha makundi yote ya jamii.
PADRI: UFISADI UKO KILA MAHALI
Padri wa Parokia Katoliki ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo la Dodoma, Lucas, aliwataka Watanzania kutambua kuwa vitendo vya ufisadi havifanywi na watu wenye majina makubwa tu, bali hata wale wenye majina madogo. Akihubiri jana kwenye ibada iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Paulo wa Msalaba mjini hapa, Lucas, alisema mafisadi wadogo wanapopata nafasi kubwa hugeuka na kuwa mafisadi wakubwa.
“Tunaposikia majina ya ufisadi tunadhani kuwa ni majina makubwa tu kwa nafasi uliyonayo unaweza kuwa fisadi mdogo,” alisema.
Alisema unapokwenda hospitali kutafuta huduma mbalimbali ama unapokamatwa na askari wa usalama barabarani na kisha kuuliza majina yao utakutana na majina yanayoonyesha kuwa ni Wakristo ama Waislamu.
Alisema wanaotuhumiwa na rushwa, hongo na dawa za kulevya, ni watu wenye imani jambo ambalo linaonyesha kuwa jamii haiishi kwa uadilifu.
Padri Lucas aliwataka Wakristo nchini kuitumia Pasaka kujitafakari, kutubu na kuishi maisha ya uadilifu.
ASKOFU: VIONGOZI WAWE WAADILIFU
Naye Askofu Sylivester Thadey wa Kanisa la International Evangelism Sinai Ipagala Dodoma, aliwataka viongozi wa chama tawala na Serikali kuwa waaminifu kwenye nafasi zao walizokabidhiwa ili waheshimiwe na jamii. Askofu Thadey alisema Watanzania hivi sasa wamefika mahali kutokuwa na imani na viongozi waliokabidhiwa madaraka kutokana na kujilimbikizia mali na ubinafsi.
Aidha, alisema viongozi hao wamekosa uaminifu na heshima. Alizitaja kashfa hizo kuwa ni pamoja na rushwa, ufisadi, ubinafsi unyanyasaji sehemu za kazi na udanganyifu jambo ambalo hata Mungu mwenyewe huchukizwa. Alisema ili waweze kurudisha imani hiyo iliyotoweka kwa Watanzania, wanapaswa kutubu mbele za Mungu kama walivyokubali kuapa kwenye kiapo cha uaminifu walipokabidhiwa madaraka ya kuwatumikia Watanzania.
"Kama walivyokuwa wameapa mbele za Mwenyezi Mungu na kukubali kuwatumikia watu kwa uaminifu na ndivyo wanastahili kutubu kwa kwenda kinyume na kiapo,” alisisitiza.
MDEGELLA ATAFSIRI KUJIVUA GAMBA
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Owdenberg Mdegella, ameitafsiri falsafa ya ‘kujivua gamba’ inayotumiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba kisayansi ni hatua ya nyoka kupata madhara ya kiafya baada ya kupita katika vumbi na kuziba masiko yake.
Akitetea hoja hiyo kisayansi, alisema kwamba nyoka hutegemea ngozi yake kama masikio katika ulinzi wake na mapito yake ndio maana anapopata madhara hutafuta njia ya kujiokoa.
Alisema kuwa kisayansi nyoka husikia kwa kutumia ngozi yake na mara anapopita katika vumbi, masikio yake huziba ndio maana hukimbilia kuvua gamba lake ili aweze kupata kusikia kwa usikivu.
Askofu Mdegella alikuwa akihubiri jana katika maadhimisho ya sikukuu ya Pasaka yaliyofanyika Kanisa kuu la Cathedral mjini Iringa.
“Kuna huu msemo wa siku hizi huko mitaani wa kujivua gamba, Niwaambie tafsiri yake, kisayansi ni kwamba asili yake ni nyoka…Kiumbe huyu hujivua gamba baada ya kupita katika vumbi na masikio yake kuziba ndio maana hufikia uamuzi wa kujivua ili apate kusikia,” alisema askofu huyo bila ya kuendelea kutoa ufafanuzi kama alikuwa akimaanisha kitu gani kupitia mfano huo huku akisisitiza kuwa wapo wenye nafasi zao watalizungumzia hilo.
Neno la kujivua gamba liliibuliwa wakati wa vikao vya CCM mjini Dodoma hivi karibuni baada ya Sekretarieti na Kamati Kuu (CC) kujiuzulu na kuundwa upya ukiwa ni mkakati wa kukirejesha chama hicho katika maadili ili kurudisha imani ya wanachama wake na umma kwa ujumla.
SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA
Kanisa la Katoliki Jimbo la Zanzibar, limesema matarajio ya wananchi kuhusu serikali ya umoja wa kitaifa (GNU) huenda yasifikiwe kutokana na kukosekana nia ya dhati ya kutaka mabadiliko.
Askofu Shao alisema wananchi wengi Zanzibar hawajaona nia ya dhati ya kutaka mabadiliko na serikali ya umoja wa kitaifa kuwa tayari kupokea mawazo na changamoto katika kuharakisha maendeleo ya wananchi wake. Alisema wananchi walitarajia kuona nguvu mpya, ubunifu mpya, na vipaji tofauti katika mwendo wa serikali kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa.
“Tunachoshuhudia zaidi ni mabadiliko ya nafasi ambazo mara nyingi haiongezi tija, sawa na mwalimu aliyemzembe kumpa adhabu ya kumhamisha kutoka shule moja kwenda shule nyengine,” alisema.
Alisema wananchi walitarajia kungekuwepo na mabadiliko makubwa katika muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa na sio mabadiliko ya kuhamisha viongozi kutoka nafasi moja hadi nyengine.
“Kwa kusoma alama na matukio machache tunaweza kusema kuwa mataraijio tuliyoyatarajia kwa kiwango kikubwa huenda yasifikiwe kwa sababu tulitarajia kuona nguvu mpya,” alisema.
Askofu huyo alisema wakati umefika kwa serikali kuwabana wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa kulipa kodi badala ya kuwabana wafanyabishara wadogo wadogo na wakulima.
Alisema maendeleo hayawezi kupatikana kwa serikali kutegemea kodi ya wafanyabishara wadogowadogo badala ya kuwabana matajiri.
Aidha, alisema inasikitisha wakati wananchi hawapati huduma zinazostahiki, lakini wapo baadhi ya viongozi wakihusiswa na matumizi mabaya ya fedha za umma.
MFUMUKO WA BEI
Kasisi Kiongozi wa Kaniasa Anglikana Zanzibar, Emmanuel Michael, alisema wakati umefika kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kushughulia tatizo la mfumuko wa bei za vyakula kwa vitendo.
Alisema hali ya maisha ya wananchi zimekuwa ngumu Zanzibar kutokana na kupanda kwa bei za mafuta kila mara na kinasababisha bidhaa kupanda bei.
PASAKA ITUMIWE KUOMBA AMANI
Jamii imeaswa kutumia sikukuu ya Pasaka kwa kuliombea Taifa lipate amani kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Changamoto myingine kwa Taifa imeelezwa kuwa ni mjadala wa Katiba mpya ya nchi inayoendelea kwa sasa na kuyahusisha makundi yote ya jamii. Hayo yalisemwa na Mchungaji Idan Kamote wa Mtaa wa Mtakatifu Barnaba Kanisa la Anglikana Kange, jijini Tanga alipokuwa akitoa mahubiri ya Pasaka.
Alisema kuwa katika kipindi hiki kigumu ambacho Taifa limejaa dhiki na tabu jamii inapaswa kujifariji kuwa Yesu Kristo aliufia ulimwengu na hivyo alishinda kifo na kaburi hivyo kila mmoja kwa nafasi yake ana wajibu wa kudumisha upendo ili amani ipatikane.
Alisema mfano mzuri wa kutambua dhiki inayowakabili Watanzania kwa sasa ni jinsi ambavyo kumekuwa na mlundikano wa kutafuta uponyaji Loliondo kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapila na kuwataka wakristo kuyakabidhi maisha yao kwa Yesu Kristo.
“Loliondo ni mfano halisi wa kuonyesha dhiki iliyopo duniani…watu hawana msaada na wanahitaji uponyaji …na Pasaka hii tujipe nafasi ya kujihoji tunaisaidiaje jamii sisi kama kanisa,kama mtu mmoja mmoja kwa kuiga mfano wa Yesu alivyofanya kabla ya kusulubiwa kwani aliwalisha wenye njaa na kuwaponya wagonjwa,” alisema.
KUPOROMOKA MAADILI
Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Isaac Amani, alisema matumizi mabaya ya vyombo vya mawasiliano kwa kisingizio cha utandawazi ni angamizo kwa jamii na mporomoko wa maadili.
Alisema upo ulemavu wa aina nyingi ukiwemo wa ajali,kuzaliwa na kujitakiwa na kufananisha suala la kuporomoka kwa maadili na ulemavu wa kujitakia.
Alisema matumizi mabaya ya vyombo vya mawasiliano kama simu, luninga, maandishi ya udaku kwa kiasi kikubwa yameathiri tabia na maadili katika jamii,kwani vyombo hivyo huanika mambo waziwazi kama vile mtu aliyepeleka bidhaa sokoni na kusababisha kila mtu hutizama na kununua.
Alisema matokeo yake ni watu wazima, vijana na watoto kuvutiwa na mambo ya kigeni yenye kuchanganya akili na kuvuruga maadili.
“Tusipotumia na kusimamia vizuri matumzi ya utandawazi kwa hekima. Hakika tutakaribisha ulemavu wa kujitakia na athari zake ni nyingi mno kwani utandawazi unakua mlezi wa jamii kwa sasa, bila kumtegemea
Mungu hakuna litakalowezekana,” alisema Askofu Amani.
Imeandikwana Edwin Agola (Dar), Godfrey Mushi (Iringa), Lulu George (Tanga), Salome Kitomari (Moshi), Sharon Sauwa na Peter Mkwavila (Dodoma), Charles Ole Ngereza (Arusha) na Mwinyi Sadallah ( Zanzibar).
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment